Na Mariam Kamgisha,Morogoro
MWENYEKITI wa Baraza la Taifa la watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi (NACOPHA), Vitaris Makuyula, amesema iwapo dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (ARVs) zitatumiwa kwa miaka mitatu mfululizo, zinazuia maambukizi mapya ya ugonjwa huo kwa mtu mwengine.
Alitoa kauli hiyo mjini Morogoro wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo na kuondoa unyanyapaa kwa viongozi wa dini na wadau wengine kwa ufadhili wa UNAIDS.
Alisema maambukizi yamekuwa yakiongezeka kutokana na watumiaji wa dawa hizo kutofuata masharti ya utumiaji wa dawa hizo.
“Hapa nieleweke kuwa mtu mgonjwa anaetumia ARV’s kwa miaka mitatu bila kuacha hata siku moja anaweza kushiriki ngono na mtu asiembukizwa bila kumuambukiza,” alisema.
Aliwataka viongozi wa dini kuzungumzia athari za unyanyapaa kwa waumini wao na kuzikemea pale zinapotokea.
“Nyinyi viongozi wa dini mna nafasi kubwa ya kukutana na waumini wengi hivyo tunaomba muwe mstari wa mbele kuhakikisha unyanyapaa unakwisha,” alisema.
Naye mshauri mhamasishaji jamii kutoka shirika la kimataifa la UNAIDS,Yeronimo Mlawa, alisema unyanayapaa na ubaguzi kwa watu wenye Ukimwi na dawa za kulevya ni kikwazo kikubwa kumaliza maambukizi mapya.