Na. Mwandishi Wetu.
Kampuni ya simu za mikononi ya Zantel leo imekabidhi hundi yenye thamani ya shilingi milioni kumi kwa chama cha Netiboli nchini msaada wenye lengo la kuendeleza mchezo huo hapa nchini.
Hundi hiyo imekabidhiwa kwa Katibu Mkuu wizara ya Habari, Vijana na Michezo, Bi Sihaba Nkinga ambaye amekitaka chama hicho kutumia vizuri msaada huo.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Afsa Biashara Mkuu wa Zantel, Bwana Sajid Khan, alisema msaada huo unalenga kusaidia aina ya maendeleo ambayo Zantel inatarajia kwenye michezo hapa nchini.
‘Mchezo wa pete ni moja ya michezo maarufu hapa nchini na yenye mashabiki wengi lakini haipati msaada wa kutosha kutoka kwa makampuni, na ndio maana Zantel tumeingia kuupa msukumo unaotakiwa’ alisema Khan.
Alisema kuwa Zantel kama mdau wa michezo nchini inatambua nafasi ya mchezo huo katika kuongeza ajira kwa vijana.
Alisema kuwa Zantel itaendelea kusaidia michezo mingine hapa nchini kama vile mchezo wa Judo, Ngumi na mingineo ambayo haitazamwi na wadhamini wengine.
Aliongeza kuwa kutokana mipango endelevu ya CHANETA Zantel inaangalia uwezekano wa kutoa msaada wa muda mrefu kwa chama hicho ili kukijengea uwezo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Bi Sihaba Nkinga mbali na kuipongea Zantel kwa msaada huo alisema kuwa ni msaada uliokuja wakati mwafaka chama hicho kikiwa kwenye harakati za kuandaa michuano ya Kimataifa.
‘Sisi kama serikali tunaipongeza Zantel kwa msaada huu na tuna hakika utasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuharakisha maendeleo ya mchezo wa Netboli hapa nchini’ alisema Nkinga.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chaneta, Ana Kibira alisema kuwa Chama chama kinaona kuwa msaada huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kufanikisha mikakati mingi ya kuinua Netiboli nchini.
Alisema kuwa Chaneta ina mikakati ya kutoa semina kwa wanachama wake pamoja na kusaka vipaji nchi nzima na msaada huo pia mbali na kusaiida michuano yao ya kimataifa itakayoanza jumamosi ijayo pia utasaidia kufanikisha malengo yao hayo.
===============