Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji (mstaafu) Joseph Warioba, amesema baadhi ya taasisi za kiserikali, ama moja kwa moja au kwa tafsiri ya mapendekezo yao , zilipendekeza au kukubali muundo wa serikali tatu.
Kwa mfano, alisema Baraza la Wawakilishi Zanzibar lilipendekeza kuwepo mamlaka huru ya Zanzibar, mamlaka huru ya Tanganyika na mamlaka ya Muungano na iwekwe wazi maeneo, uwezo, nguvu, utendaji na mipaka ya kila mamlaka.
Akiwasilisha rasimu ya katiba jana kwa Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma, alisema Baraza la Ofisi ya Makamu wa Rais lilipendekeza, kuhusu muundo wa serikali kwamba, kuwe na rais mmoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wakuu wa serikali za washirika wa muungano wapewe vyeo vingine vinavyoendana na hadhi na mamlaka zao.
Alisema baraza hilo lilisema katika kutaja serikali tatu inabidi zitenganishwe ili serikali ya Muungano ionekane ndio ya juu.
Huku akishangiriwa na wabunge,alisema Baraza la Ofisi ya Waziri Mkuu lilipendekeza, kuwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, Waziri Mkuu wa Serikali ya Tanganyika na Waziri Mkuu wa Serikali ya Zanzibar .
Aidha alisema baraza hilo lilisema mapendekezo hayo ni kwa sababu hakuna umuhimu wa kuwa na marais watatu katika nchi moja na wala neno Rais halimuongezei hadhi kiongozi yeyote.
Pia alisema Baraza hilo lilisema hali hiyo itatoa nafasi kwa Mawaziri Wakuu kuwa watendaji zaidi na hivyo kusimamia serikali za washirika.
Alisema Bunge la Jamhuri ya Muungano katika maoni yake lilipendekeza kuwepo Tume ya Utumishi wa Bunge ambayo inajumuisha, katika wajumbe wake, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano (Mwenyekiti), Spika wa Bunge la Tanzania Bara na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Akinukuu sehemu ya waraka wa Baraza la Wawakilishi uliowasilishwa Tume Februari 2013, pamoja na mambo mengine, alisema Baraza la Wawakilishi lilitoa maoni yafuatayo:“Kwa sababu Wazanzibari ni waumini wa Muungano ambao haukuondoa na hautoondoa uwepo wa Zanzibar kama nchi, ni vyema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ijayo iweke wazi kuwa Tanzania ni Jamhuri ya Muungano inayotokana na Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Hali hii itahakikisha kuwepo na maeneo maalum ya mamlaka ambayo Zanzibar ina uwezo nayo kama nchi (yaani, mamlaka ya dola ya Zanzibar ).
“Kwa sababu inapendekezwa kuwepo na mamlaka ya Zanzibar huru na mamlaka ya Tanganyika huru ndani ya Jamhuri ya Muungano, mamlaka ya Muungano iwekwe wazi – maeneo yake, uwezo au nguvu zake, na utendaji wake. Mambo yote hayo yawekwe wazi na mipaka yake,”alinukuu.
“Uwepo wa Muungano uonekane katika hali zote uundwaji wa mamlaka za Muungano, ufanyaji kazi katika mamlaka za Muungano, ufanyaji wa maamuzi katika mamlaka za Muungano, na uingizwaji na upunguzwaji katika orodha wa mambo ya Muungano,” anukuu sehemu ya waraka huo wa Baraza.
Alisema baada ya kuona takwimu hizo na kuchanganua sababu zilizotolewa na makundi mbali mbali, Tume iliamua kufanya utafiti wa kina kuhusu muundo wa muungano na matatizo yake tangu muungano ulipoundwa.
Alisema katika utafiti huo mambo kadhaa yamejitokeza, ambapo alisema kulikuwa na changamoto nyingi baada ya Tanganyika na Zanzibar kuungana mwaka 1964 na kwamba ujenzi wa taasisi za kuendesha mambo ya muungano ulikuwa ni changamoto kubwa.
Aidha alisema Serikali ya Muungano haikuwa na taasisi zake, kwa hiyo ilianza kwa kutumia taasisi zilizokuwapo katika sehemu zote mbili za muungano.
Alisema hata uamuzi wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya demokrasia ya chama kimoja ulichukuliwa wakati nchi ikiwa na vyama viwili; TANU na ASP kwa hivyo kila upande uliendesha mambo yake kutumia itikadi na sera zake.
Alisema changamoto hizo hazikuzuia kuimarika kwa muungano kwa sababu utashi wa kisiasa wa waasisi wa muungano ulikuwa mkubwa.
Jaji Warioba alisema baada ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuvunjika, baadhi ya mambo yaliyokuwa chini ya Jumuiya hiyo yaliwekwa kwenye orodha ya mambo ya muungano, matokeo yake, nchi ilionekana moja, yenye mshikamano, utulivu na amani.
“Wakati huo, viongozi na watumishi wa umma na kwenye chama cha siasa walipangiwa kazi sehemu yoyote ya nchi bila kujali sehemu wanayotoka. Kwa muda mfupi nchi ilionekana kuwa kweli ni taifa moja,lakini hali hiyo haikudumu kwa muda mrefu,utaifa wa nchi mbili ukaanza kujitokeza. Viongozi na watumishi wa umma kutoka upande mmoja wa muungano wakaonekana hawapendi kwenda kufanya kazi upande wa pili wa muungano,” alisema.
“Pia majina ya sehemu mbili za Muungano yakabadilishwa. Badala ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani tukaanza kutumia Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, ili kulinda Zanzibar isionekane imemezwa. Ni wakati huo, lugha ya Tanganyika kuvaa Koti la Muungano ilianza kusikika,” alisema.
Alisema 1984, kulitokea kile kilichoitwa “kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar ”, ambapo msingi wake ilikuwa ni mpango wa baadhi ya viongozi wa Zanzibar kutaka serikali tatu, ingawa jaribio hilo halikufanikiwa, Zanzibar ilitunga katiba mpya mwaka huo huo.
Alisema kwa maana nyingine, Zanzibar ikaanza kutumia bendera ya taifa iliyo tofauti na mwaka 1992, ikajiunga ilijiunga na (OIC) na Bunge lilipitisha azimio la kuzitaka serikali zote mbili kushirikiana katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo na matatizo mengine ya muungano na kutoa taarifa bungeni katika kipindi cha mwaka mmoja.
Alisema mwaka 1993, wakati wa mkutano wa bajeti, wabunge kutoka Tanzania Bara (G55) walipeleka bungeni hoja ya kuundwa kwa serikali ya Tanganyika, hoja ambayo ilipitishwa, hata hivyo Novemba 1993 kikao maalum cha CCM kilichofanyika Dodoma kilifikia muafaka kwamba azimio hilo la bunge lisitekelezwe.
Alisema Tume yake iliamua kufanya uchambuzi wa kina kuhusu baadhi ya malalamiko, hasa malalamiko ya Zanzibar kwa sababu malalamiko ya Tanzania Bara kuhusu Muungano yanatokana, kwa kiwango kikubwa na hatua zilizochukuliwa kwa upande wa Zanzibar .
Alisema kama malalamiko ya Zanzibar yakipatiwa ufumbuzi, malalamiko ya Tanzania Bara nayo yatakuwa yamepatiwa ufumbuzi.
Alisema katika kuchambua malalamiko ya Zanzibar kwamba Tanganyika imevaa koti la Muungano, Tume imebaini kwamba muundo wa sasa wa muungano umeifanya Serikali ya Muungano, kwa kiwango kikubwa, kushughulikia zaidi mambo ya Tanzania Bara, hasa mambo ya maendeleo ikiwemo kilimo, elimu, afya, maji, nishati na madini, ujenzi, uchukuzi, maliasili na utalii.
Alisema wakati wa kikao cha bajeti, bunge la muungano hutenga siku mbili au tatu za majadiliano kwa wizara zinazosimamia mambo hay ya Tanzania Bara wakati mambo ya Muungano kama vile ulinzi, mambo ya nje na mambo ya ndani hutengewa siku moja au nusu siku.
“Sheria nyingi zinazotungwa na bunge zinahusu mambo ya Tanzania Bara. Maswali ya wabunge kuhusu mambo ya maendeleo pia yanahusu Tanzania Bara na ziara za wabunge kukagua miradi ya maendeleo zinahusu Tanzania Bara katika mambo yasiyo ya Muungano,” alisisitiza.
Alisema hali hii ndiyo imeifanya Tanganyika ionekana imevaa koti la muungano.
Akizungumza kwa kujiamini alisema hata Rais wa Jamhuri hafanyi ziara za kukagua miradi ya maendeleo na kutoa ahadi kwa upande wa Zanzibar .
“Sura ya Serikali ya Muungano inaonyesha kuegemea zaidi upande wa Tanzania Bara. Kati ya Wizara 24 ni wizara mbili tu ndizo zinazoshughulikia mambo ya Muungano pekee. Wizara kumi zinashughulikia mambo ya Tanzania Bara na Wizara kumi na mbili zinashughulikia mambo mchanganyiko ambayo mengi ya mambo hayo yanahusu Tanzania Bara. Kwenye utawala, viongozi wakuu wengi wa Wizara wanatoka Tanzania Bara,” alisema.
Alisema hivi sasa ni Katibu Mkuu mmoja tu ndiye anayetoka Zanzibar na kwamba hali hiyo inatokana na ukweli kwamba serikali ya Muungano inashughulikia zaidi mambo yasiyo ya Muungano na ndiyo imeifanya Tanganyika kuonekana imevaa koti la Muungano.
Alisema eneo jingine lenye matatizo ni mgongano kati ya katiba ya Muungano na katiba ya Zanzibar .
Alisema ibara ya 132 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 imeweka masharti kwamba sheria zinazotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano hazitatumika Zanzibar hadi zipelekwe Baraza la Wawakilishi.
Alisema jambo hilo limeleta mgongano wa katiba na juhudi zilizofanywa na pande zote mbili hazikufanikiwa kuondoa mgongano huo.
Katika muafaka wa mwaka 1994, alisema serikali zote zilikubaliana kwamba Zanzibar ifanye mabadiliko kwenye katiba yake ili mgongano huo uondolewe lakini adi sasa muafaka haujatekelezwa.
Aidha alisema mabadiliko ya katiba ya Zanzibar katika ibara ya kwanza yaliyofanywa mwaka 2010 yametamka wazi kwamba Zanzibar ni nchi kati ya nchi mbili zinazounda Muungano wakati katiba ya Jamhuri inaelekeza kwamba Tanzania ni nchi moja.
Alisema mabadiliko ya katiba ya Zanzibar pia yamehamisha baadhi ya madaraka ya Serikali ya Muungano kwenda Zanzibar .
Kwa mfano, alisema katiba ya Jamhuri inampa Rais wa
Jamhuri madaraka ya kuigawa nchi katika maeneo lakini katiba ya Zanzibar imeyahamisha madaraka hayo kwenda kwa Rais wa Zanzibar .
Alisema wakati wa kukusanya maoni ya wananchi, Tume ilibaini haitakuwa rahisi kubadili katiba ya Zanzibar kuifanya Zanzibar kuonekana kuwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano badala ya kuwa na sura ya nchi.
Mabadiliko ya aina hiyo alisema yatahitaji kura ya maoni kama katiba ya Zanzibar inavyoelekeza na kwamba ni dhahiri uwezekano wa kufanya mabadiliko kwenye katiba ya Zanzibar ili Zanzibar iwe sehemu ya nchi moja badala ya kuwa nchi, ni mdogo sana .