Na Fatuma Kitima, DAR ES SALAAM
RAIS mstaafu wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Ali Hassan Mwinyi,amewaasa waislamu kuzitambua fursa zilizopo na kuzitumia kwa umakini ili waweze kunufaika nazo hasa suala zima la kiuchumi.
Hayo aliyasema jana jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa kongamano la Mashekh na Wanazuoni linalojadili mfumo wa uchumi wa kiislamu kwa mujibu wa Qur-an na Sunnah za Mtume (S.A.W) na changamoto zake.
Amewashauri Waislamu na wasiokuwa waislamu kujiunga na Saccos, Vicoba, pamoaj na vikundi vingine vya kiuchumi,kuangalia namana ya kukuza uchumi wao na wananchi kwa ujumla.
Alisema kujifunza uchumi wa kimagharibi ambao unapanda na kushuka,hivyo bila kuelimishana na kuwa na uelewa itakuwa vigumu watu kufahamu mfumo wa kiuchumi kwa misingi ya kiislamu.
Naye Mwenyekiti wa kongamano hilo,Shekh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Salum, ametoa wito kwa walimu wanaofundisha watoto madrasa, kutoa elimu inayostahili ili kuwajengea vijana uelewa mzuri wa kutumia fursa zilizopo za kiuchumi.
Aliwataka Waislamu na wasiokuwa waislamu kutumia fursa za kibenki za kiislamu zinapotokea kwani benki hizo ni za watu wote na sio jamii fulani pekee.
Kongamano hilo limeandaliwa na Taasisi ya Walimu wanaofundisha Qur-an Tanzania (JUWAQUTA).