Na Hassan Hamad OMKR
Baraza la Manispaa la Zanzibar limeshauriwa kuweka utaratibu unaofaa kuhakikisha kuwa mrundikano wa taka hasa katika maeneo ya mjini unapungua.
Wito huo umetolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, wakati alipofanya ziara ya kutembelea baadhi ya majaa ya Mkoa wa Mjini Magharibi, soko la matunda Mombasa, pamoja na kutembelea shimo la kutupia taka lililoko Kibele, kujionea hali halisi ya ukusanyaji na utupaji wa taka taka.
Amesema ni muhimu kuhakikisha kuwa taka zinakusanywa katika maeneo yaliyotengwa na kutupwa kwa wakati, ili kupunguza mrundikano wa taka unaoleta taswira mbaya kwa mji wa Zanzibar, samba na uwezekano wa kutokea maradhi ya mripuko hasa katika msimu huu wa mvua unaoendelea.
Katika kufanikisha suala hilo, Maalim Seif amehimiza mashirikiano ya wananchi kwa kuepuka kuwatuma watoto kupeleka taka jaani, ambao kwa kawaida hawazipeleki katika eneo linalostahiki, hali inayochangia uchafuzi wa mazingira katika maeneo hayo.
Aidha Makamu wa Kwanza wa Rais ameuagiza uongozi wa Baraza la Manispaa kuangalia uwezekano wa kufanya kazi za usafi na utupaji wa taka nyakati za usiku, ili kuepusha usumbufu unaojitokeza wakati wakitekeleza majukumu yao ya kila siku.
Amesema hatua hiyo pia italiwezesha baraza hilo kufanya kazi zaidi na kwa ufanisi, ikizingatiwa kuwa foleni za magari hupungua, hasa kwa vile eneo la kutupia taka limetengwa mbali na mji.
Nae Mkurugenzi wa Manispaa ya Zanzibar Abeid Juma, amesema kazi za usafi na utupaji wa taka zimekuwa zikizorota kutokana na upungufu wa vifaa vikiwemo magari na vikapu vya kubebea taka hizo.
Hata hivyo amesema tatizo hilo linaweza kupungua mara tu watakapopata vifaa hivyo vinavyotarajiwa kupatikana mwezi wa Septemba mwaka huu.
Amefahamisha kuwa kwa ujumla wanayo maeneo yapatayo 42 ya kutupia taka katika manispaa ya Zanzibar, lakini tatizo kubwa ni upungufu wa magari, hali inayopelekea kuchelewa kuondolewa kwa taka hizo na kuleta usumbufu kwa wananchi na wageni.
Aidha Mkurugenzi huyo ameutaka uongozi wa soko la matunda Mombasa, kutengenisha taka za kawaida na zile zitokanazo na samaki, ili kuepusha harufu mbaya inayojitokeza katika soko hilo, kama lilivyofanikiwa kwa soko kuu la Darajani.
Wakati huo huo Maalim Seif ametembelea kituo cha mafunzo ya kilimo cha mboga mboga na matunda kilichoko Dimani, na kujionea teknolojia mpya ya kilimo hicho.
Amesema iwapo kilimo hicho kitaendelezwa na kuwawezesha wakulima kupata mikopo, Zanzibar inaweza kuondokana na tatizo la uagiziaji wa mazao hayo, na hatimaye kuweza kusafirisha nje ya nchi.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Mali asili, Affan Othman Maalim amesema kituo hicho kimeanza kutoa mafunzo kwa maofisa wa kilimo, mabwana na mabibi shamba, ili nao waweze kusambaza taaluma kwa wakulima.
Amesema licha ya kilimo hicho kuwa na gharaka kubwa za kuanzia, lakini gharama hizo zinaweza kulipwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu na kuongeza pato la wakulima.
Ameahidi kuwa teknolojia hiyo ya kilimo itawafikia wakulima wa maeneo yote Unguja na Pemba, na kuweka utaratibu wa kuratibu mikopo, ili wakulima waweze kunufaika na kilimo hicho.