Na Joseph Ngilisho,ARUMERU
DIWANI wa kata ya Olkiding'a,Samweli Ngarabani,amenusurika kuuawa na wananchi wenye hasira kali, baada ya kuwatolea majibu machafu kwenye mkutano wa hadhara aliouitisha kwa lengo la kuhamasisha uchangiaji wa mradi wa ujenzi wa maabara katika skuli ya sekondari Olkiding'a.
Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki katika kijiji cha Olgoruno,Olkidinga,wilayani Arumeru,baada ya kuwataka wananchi hao kuchangia shilingi 60,000 kila mmoja,kiwango walichodai ni kikubwa ikilinganishwa na hali zao za maisha.
Hali hiyo ilisababisha vurugu kubwa kutoka kwa wananchi hao na baadhi yao kutaka kumshambulia kwa siraha.
Kilichowakasirisha wananchi hao ni baada ya mmoja wa wananchi kuhoji fedha za miradi ya maji na chumba cha kompyuta alizowachangisha kipindi cha nyuma huku wakimhoji kwanini amekuwa akiibuka tu wakati wa michango na baadae haonekani katika kata hiyo,kusikiliza kero za wananchi.
Diwani huyo alijinasibu kwa kutamka kuwa watake wasitake lazima wachangie maendeleo ya kata hiyo huku akitamba kuwa ameagizwa na rais kusimamia michango hiyo na kuwatisha kuwa iwapo mwananchi yeyote atakayekaidi agizo hilo atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.
“Mkikataa mimi sitishwi na hilo na suala la maendeleo ni lazima mtachangia mtake mstake,tutawachukulia hatua za kisheria ,hili ni agizo la rais Kikwete,” alisema.
Kauli ya diwani huyo ilionekana kuwaudhi na kuwatia hasira wananchi hao ambapo baadhi ya vijana walianza kumzonga wakimtaka aondoke kwenye kata hiyo,huku wengine wakinyanyua silaha za jadi wakimtishia kumkatakata,lakini alilazimika kuwaomba msamaha kwa kuwapigia magoti huku akiwatuliza wasimdhuru.
Hata hivyo, mkutano huo kuvunjika baada ya wananchi kuanza kupiga kelele wakidai hawezi kuchangia chochote mpaka wasomewe mapato na matumizi ya kijiji hicho wakidai hawakuwahi kusomewa tangu mwaka 2009.
Naye Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Sarah Mollel, alikiri kutosoma mapato na matumizi katika kipindi kirefu,hata hivyo alieleza kuwa Mtendaji aliyekuwepo kabla aliondoka na nyaraka za ofisi hiyo na kwenda nazo kata ya Odonyosambu alikohamishiwa,hivyo hana kumbukumbu yeyote juu ya mapato na matumizi ya kijiji.