Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar 03/04/2014
Kampuni ya Royal Hanskoning DHV ya Nchini Uholanzi inayoendelea na Utafiti wa kujua Maeneo ambayo yanafaa kujengwa Bandari imegundua Maeneo ya Fumba, Mangapwani na Maruhubi ni maeneo muhimu ambayo yanaweza kujengwa bandari za kisasa.
Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Elzinga Theun amesema hatua za awali za utafiti wao zinaonesha maeneo hayo ya Kisiwa cha Unguja ni mazuri kwa Ujenzi wa Babandari kutokana na kuwa na kina kizuri cha maji na kukosekana kwa mawimbi Makali.
Theun ameyasema hayo leo katika Semina ya kujadili maendeleo ya Sekta ya Bandari iliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Serena Mjini Zanzibar.
Amefahamisha kuwa katika Tafiti zao wamegunduwa kuwa maeneo ya Mashariki ya Kisiwa cha Unguja yana changamoto nyingi za Ujenzi wa Bandari ikiwemo ile ya Mawimbi makali ya bahari jambo ambalo linaweza kuleta shida.
Aidha Mkurugenzi Theun ameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutafuta mbinu za kuitanua Bandari ya Malindi ili iweze kuhimili mahitaji yaliyopo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar Dkt Juma Malik Akili amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kufikiria namna ya kuitanua Bandari ya Malindi ili kuhakikisha inakidhi Viwango vinavyotakiwa.
Amesema kabla ya kuanza Ujenzi wa Bandari Mpya ya Maruhubi Serikali inatafuta eneo la kuweka Makontena zaidi ya Laki mbili kwa mwaka ifikapo mwaka 2017 badala ya uwezo wa kuweka Makontena Elfu 60 uliopo sasa.
Dkt Akili amesema hatua hiyo itaisaidia Zanzibar kupiga hatua kubwa katika maendeleo ya Bandari na kuufanya uchumi wa Zanzibar kukua kwa kiwango kikubwa.
Utafiti huo unaofanywa na Kampuni ya Royal Hanskoning DHV ya Nchini Uholanzi wa kuchunguza maeneo mazuri ya kujenga Bandari katika Visiwa vya Unguja na Pemba unatarajiwa kugharimu Jumla ya Pounds Laki 1.5 za Uengereza ambapo gharama hizo zimetolewa na Serikali ya Uholanzi.