Jambo linalosemwa mara nyingi ni marekebisho ya kumi ya Katiba ya Zanzibar ambayo yanadaiwa kwenda kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Suala hilo limezusha mjadala mkubwa Tanzania Bara ambako inaonekana wamechukizwa na Katiba ile kutamka kwamba Zanzibar ni nchi inayounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ni wazi kuwa siyo sahihi kulaumu Katiba ya Zanzibar kuwa imekosea kutamka kuwa visiwa hivyo ni nchi, kati ya nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kifungu kinacholalamikiwa ni sura ya 1(1) inayoeleza Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na visiwa vidogo vilivyozungukwa na bahari yake kama ilivyokuwa kabla ya 1964.
Zanzibar ina serikali yake ambayo ni wazi kuwa inahitaji kuwa na sheria, watu, ardhi na mipaka kwani bila ya mambo hayo serikali hiyo inafanyaje kazi wakati hata mipaka ya eneo lake haijulikani?
Nguvu ya SMZ
Mipaka ya nguvu za SMZ kikatiba haina lengo la kupokonya mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Jiulize, SMZ itawezaje kutekeleza sheria zake ikiwa eneo la mipaka yake haikuainishwa katika katiba?
Kwa mfano, kuna meli inapita katika eneo la pwani ya Zanzibar baina ya Tanzania Bara na Zanzibar, lakini ilivyo meli hiyo ipo eneo la Zanzibar, ikamwaga mafuta machafu na kuchafua mazingira. Je, sheria ipi inatumika katika kuishtaki meli hiyo wakati suala la usajili wa meli siyo la Muungano?
Mfano mwingine ni kuwa kuna mtu amekamatwa na Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM) akiwa na jahazi eneo la pwani ya Zanzibar akisafirisha karafuu kwa magendo, ni sheria ipi itatumika ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au ya Zanzibar?
Jawabu ni sheria ya Zanzibar. Sasa, je sheria hiyo mipaka yake inaishia wapi kama katiba haikuweka eneo la utawala wa Zanzibar?
Kwa maana hiyo, mtuhumiwa atashinda kesi kwa hoja nyepesi kuwa mipaka ya Zanzibar haifahamiki, kwa hivyo hakufanya kosa kwa sababu alikuwa haelewi wapi mipaka hiyo inaanzia na kuishia kwa kuwa haipo?
Suala la mafuta na gesi asilia limeamualiwa kuwa liondolewe katika orodha ya mambo ya Muungano kwa maana hiyo kila upande utasimamia kwa sheria zake, ikiwa hivyo ndivyo ni lazima eneo la mipaka ya kila upande ifahamike maana hakuna mwekezaji atakayekuja Zanzibar kufanya utafiti wa mafuta ikiwa eneo la mipaka yake haikuwekwa wazi.
Kwa kuwa suala la uchumi siyo la Muungano kwa maana ya kila upande una wizara yake inayoshughulikia uchumi, mipango na sera zake za uchumi na bajeti yake ni lazima iwepo mipaka ya eneo la Zanzibar kwani wawekezaji wa miradi mikubwa hawataweza kuwekeza miradi yao katika hali ya kutofahamika mipaka ya utawala wa Zanzibar.
Pia, baadhi ya watu wamekuwa wakijenga hoja kwamba Katiba ya Zanzibar katika mabadiliko yake ya kumi yamempa uwezo Rais wa Zanzibar kuigawa nchi katika mikoa na wilaya, kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hii, pia ni hoja ambayo imeshapitwa na wakati. Mantiki ya kuwekwa kifungu hicho katika Katiba ya mwaka 1977 ilitokana na ukweli kwamba wakati huo kulikuwa na mfumo wa chama dola ambao makatibu wa CCM wa mkoa ndiyo hao hao waliokuwa wakuu wa mikoa kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye alikuwa mwenyekiti wa CCM.
Jamhuri ya Tanganyika na ile ya Watu wa Zanzibar ziliungana mwaka 1964 na ilipofika 1965 kulipitishwa kwa Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Chini ya katiba hiyo, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikawekwa chini ya utawala wa chama kimoja cha siasa, ingawa vilikuwa viwili, Zanzibar kulikuwa na Afro Shiraz Party na TANU kwa Tanzania Bara.
Kwa kuwa suala la vyama vya siasa halikuwa katika orodha ya mambo ya Muungano, vyama viwili ndivyo vilivyosalia hadi ilipofika mwaka 1977, ASP na TANU vilipounganishwa na kuzaliwa CCM.
Nadharia ya chama kushika hatamu iliendelea na katika mfumo huo mihimili yote ya serikali ilikuwa chini ya chama kimoja na ndipo katika katiba ya mwaka 1977 makatibu wa CCM wa mikoa ndio hao hao waliokuwa wakuu wa mikoa.
Kama watu wanadai kuna ukiukwaji umefanywa na Katiba ya Zanzibar, jambo moja wanalotakiwa kuelewa ni kuwa hakuna katiba ndogo wala kubwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Zanzibar siyo jimbo
Zanzibar siyo jimbo kama yalivyo majimbo katika nchi ya Australia au India ambapo zinaonyesha majimbo na hazitakiwi kukiuka katiba.
Mfano hai ni kuwa hadi kufikia mwaka 2010, wakuu wa mikoa waliendelea kuwa wajumbe wa BLW Zanzibar wakati Tanzania Bara, wakuu wa mikoa hawakuwa tena wabunge.
Suala la pili ni kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anapoteua wakuu wa mikoa na wilaya pamoja na makatibu tawala wa mikoa na wilaya anafanya hivyo kwa ile ya Tanzania Bara na siyo Zanzibar.
Tatu, Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ndiye anayeteua wakuu wa mikoa na wilaya pamoja na maofisa tawala wa mikoa na wilaya na sina hakika kama ipo siku kabla ya kuwateua aliomba idhini au kushauriana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uteuzi wa nafasi hizo.
Ieleweke wazi kuwa Zanzibar siyo jimbo la nchi yeyote badala yake ni nchi, ina watu wake na sheria zake kwa mujibu wa mkataba wa Muungano wa mwaka 1964 ambao umelinda Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Serikali yeyote ile lazima iwe na eneo lake la utawala ambalo limeelezwa katika katiba ya hiyo nchi. Kiini cha tatizo hili la sasa kuhusu Zanzibar na katiba yao ni ukiukwaji uliofanywa makusudi wa mkataba wa Muungano wa mwaka 1964.
Tusikwepe ukweli, watu wa kulaumiwa katika hali iliyopo sasa ni wale waliochangia au kusababisha kero za Muungano na kwa sababu hiyo sioni kama tunaweza kuepuka kuwa na muundo wa Muungano wa serikali tatu.
Chanzo - Mwananchi