Na Hafsa Golo
MELI mpya ya serikali inayotengenezwa nchini Korea Kusini inatarajiwa kuwasili nchini Febuari 15 mwakani.
Meli hiyo inayotengenezwa na kampuni ya Posco Plantec, ipo katika hatua nzuri ya ujenzi wake na itakuwa na uwezo wa kuchukua abiria 1200 na mizigo tani 120.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Meli Kepteini, Alhaj Masoud Sururu, alisema wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Malindi.
Alisema kupatikana kwa meli hiyo kutaondosha usumbufu kwa wasafiri wa Pemba na Unguja.
Alisema meli hiyo ina uwezo wa kupambana na mawimbi makali wakati wa safari hasa katika mkondo wa Nungwi na itakuwa inachukua muda wa saa nne kutoka Unguja hadi Pemba na masaa matatu kwa Unguja hadi Dar esSalamu.
Aliwahakikishia wananchi kwamba nauli ya meli hiyo itakuwa nafuu tofauti na boti nyengine zinazomilikiwa na watu binafsi.
Akielezea kuhusu meli ya Mv Maendeleo alisema kutokana na uchakavu unaoikabili meli hiyo haitochukua tena abiria na badala yake itakuwa meli ya mizigo na itafanya safari zake kati ya Unguja, Pemba, Tanga na Dar es Salamu.
Akizungumzia kuhusu wafanyakazi wa meli hiyo mpya alisisitiza kuwa kwa hivi sasa shirika lina wafanyakazi wa kutosha hata hivyo kama litaamua kuajiri wafanyakazi wapya kipaumbele kitatolewa kwa makapteni na mainjinia.