Na Juma Khamis
ILI kuchangia sekta ya utalii inayozidi kukua kwa kasi nchini, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), kitaanzisha shahada ya kwanza ya usimamizi wa utalii na biashara (B.TMM) katika mwaka wa masomo 2014/2015.
Akizungumza katika mkutano wa wadau kuchambua mtaala utakaotumika katika shahada hiyo uliofanyika kampasi ya SUZA Vuga, Makamu Mkuu wa SUZA, Prof. Idris Rai, alisema lengo la SUZA ni kuchangia katika kuimarisha uchumi kupitia sekta muhimu ukiwemo utalii.
Alisema shahada hiyo itakidhi mahitaji ya ushindani uliopo katika sekta ya utalii.
Aidha, alisema wanafunzi watakaosoma shahada hiyo baadae watapata nafasi ya kusoma shahada ya pili katika masuala ya usimamizi wa biashara na kuwa mameneja wa hoteli.
Hali hiyo itawasaidia watu wengi kufaidika na kuchangia katika sekta ya utalii.
Kaimu Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Jamii, Idrisa Haji, alisema kozi hiyo mpya itasaidia kupunguza kilio cha muda mrefu cha Wazanzibari kwamba nafasi za juu katika miradi ya hoteli zinachukuliwa na wageni.
Alisema kwa kuanzia chuo kinalenga kudahili wanafunzi 40-50 lakini idadi itaongezeka kila mwaka wa masomo.
Kuhusu wahadhiri, alisema chuo kinapanga kuajiri wataalamu wa kusomesha shahada hiyo ambao watashirikiana na wale waliopo sasa.
Mkutano huo uliwashirikisha wadau muhimu katika sekta ya utalii, wakiwemo wamili wa hoteli, watembeza watalii, Kamisheni ya Utalii, mtaalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na taasisi nyengine muhimu.