Na Khamisuu Abdallah
BOSI aliemmwagia maji ya moto mfanyakazi wake wa ndani na kumsababishia maumivu, amefikishwa mahakamani na kurejeshwa rumande hadi Aprili 22.
Mshitakiwa huyo ni Ali Abrahman Ali (49) mkaazi wa Kwamtipura wilaya ya mjini Unguja.
Hati ya mashitaka iliyowasilishwa mahakamani na Mwendesha mashitaka, Said Ali mbele ya hakimu Nayla Abdul-basit Omeiya, mshitakiwa alipatikana na kosa la shambulio la hatari ambapo ni kinyume na kifungu 225 sheria namba 6 ya mwaka 2004 sheria za Zanzibar .
Ilidaiwa bila ya halali, alimshambulia Tausi James Lumnyija ambae ni mfanyakazi wake wa nyumbani (house girl) kwa kummwagia maji ya moto mwilini mwake na kumsababishia maumivu.
Tukio hilo lilidaiwa kutokea Machi 15 mwaka huu majira ya saa 5:00 asubuhi Kwamtipura wilaya ya mjini Unguja.
Awali mshitakiwa huyo aliposomewa shitaka lake alikana na kuiomba mahakama impatie dhamana yake mwenyewe ombi ambalo lilipingwa na upande wa mashitaka.
Mwendesha Mashitaka aliiambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kutajwa huku wakiendelea na upelelezi.