Na Fatuma Kitima,DAR ES SALAAM
TAKWIMU zinaonesha Watanzania milioni 16 hadi 18 wanapata ugonjwa wa malaria kila mwaka na inakadiriwa kwamba watu 100,000 hufariki kwa ugonjwa huo ikiwa kati yao 70,000 ni watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
Taarifa hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Meneja miradi wa chuo kikuu cha John Hopkins,Waziri Nyoni, wakati akitoa mada ya Tuungane kutokomeza malaria kwa waandishi wa habari.
Alisema kwa Tanzania takwimu zinaonesha kila baada ya dakika tano, mtoto mmoja hufariki kwa ugonwa huo na kwa Afrika watoto hufariki kila baada ya sekunde 60 hivyo ugonjwa huo usababisha uchumi wa nchi kushuka.
Aidha alisema ugonjwa huo husababisha mahudhurio madogo skuli,kupunguza nguvu kazi katika uzalishaji sehemu za kazi na familia kupoteza pesa nyingi kwa kumtibu mgonjwa.
Kwa mujibu wa shirika la Afya Duniani (WHO), tatizo hilo ni la dunia nzima na maskini ndio waathirika wakubwa.
Aidha alisema tafiti zinaonyesha, uchumi na kijamii Afrika pekee malaria inakadiriwa kugharimu dola za Marekani billioni 12 kwa mwaka, katika suala zima la kujikinga,kutoa elimu, pamoja na fedha za kujikimu watoa huduma.
Naye Balozi wa malaria nchini, Leodegar Tenga, aliyaasa makampuni ambayo hayajajiunga na kampeni hiyo na Watanzania kwa ujumla kutoa mchango wa aina yoyote unaolenga kutokomeza ugonjwa huo.
“Nasema hivyo kwa sababu, bado ni ugonjwa unaoua watu wengi kuliko magonjwa mengine, huku ukituathiri kwa namna moja au nyingine. Kwa mfano wakati nikianza skuli miaka ya 1960, tulikuwa wanafunzi 18 darasani, na leo hii tumebaki sita,” alisema.
Tenga alisema kati ya wenzake 12 waliokwishafariki, wanafunzi 11 walifariki kutokana na malaria.
Hadi sasa kampuni 37 zimejiunga na kampeni hiyo ya malaria safe initiative, yakiwemo ya Tanzania Breweries Limited (TBL) na kampuni ya simu za mkononi ya Zantel.