Na Ramadhan Himid , China
WASHIRIKI wa semina ya usimamizi wa sheria za bahari kutoka nchi tofauti za Afrika walioko mjini Ningbo China, wametakiwa kila mmoja kujenga utamaduni wa kuheshimu utamaduni wa mwenzake kwa kuwa kila nchi ama kabila lina utamaduni wake uliouzoea.
Hayo yalielezwa na mwasilishaji na kamanda wa ngazi za juu wa chuo cha wanamaji wa jeshi la polisi China, Prof. Mao Yongquan, wakati akielezea utamaduni wa watu wa China jinsi unavyoweza kufanana ama kutofautiana na nchi nyengine za Afrika na ulimwengu kwa ujumla.
Alisema utamaduni ni mfumo mzima wa maisha namna watu walivyojipangia kuishi na hivyo basi hakuna utamaduni wa mtu ulio bora kuliko mwengine bali kuna kutofautiana na la muhimu kila mmoja kuheshimu utamaduni wa mwenzake.
“Najua mmetoka barani Afrika, kwa vyovyote vile tutatafautiana kila mmoja kati yetu nanyi kwa lugha, imani, chakula, kivazi na hata kutoa lugha ya ishara ni kila mmoja na vile alivyozoea na kwa mantiki hiyo tumeona ni vyema kabla ya kuanza kwa semina hii tukaelezana utamaduni wetu ulivyo kwa lengo la kuvumiliana kati yetu, tukishaelewa hilo najua tutakwenda vizuri,” alisisitiza Prof. Mao
Aliwaambia wanasemina hao kwa kunukuu usemi wa lugha ya kiengereza unaotafsirika kama “ukiwa nchi ya Roma, fanya kama Waroma wanavyofanya” ili uweze kwenda nao sambamba kama wasemavyo waswahili “ukienda nchi za wenye chongo huna budi jicho lako moja kulifumba.”
Washiriki hao pia mbali na kujifunza historia na utamaduni wa kichina pia walianza kufunzwa lugha ya Kichina ili iwe rahisi kuwasiliana na jamii inayowazunguka angalau kwa kutoa salamu.
Mafunzo hayo ya wiki tatu yanayohusu namna ya kukabiliana na matukio makubwa ya kihalifu kwenye bahari pamoja na maafa yake yameshirikisha jumla ya washiriki 20 wanaozungumza lugha ya kiengereza barani Afrika kwa kada tofauti kama polisi, jeshi, mahakama, mamlaka za bahari na uvuvi kutoka nchi tisa za Tanzania, Misri, Eritrea, Ghana, Liberia, Mauritius, Nigeria, Siera Leone na Sudan.
Aidha, mafunzo hayo yanadhaminiwa na chuo cha wanamaji wa jeshi la polisi nchini China yanatarajiwa kufunguliwa rasmi Aprili 10 mwaka huu na Rais wa chuo hicho, Yang Jun.