Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

UZINDUZI WA MFUMO WA UWASILISHAJI WA MALALAMIKO KWA NJIA YA UJUMBE WA SIMU YA KIGANJANI

$
0
0
Na Ramadhani Ali , Maelezo Zanzibar.
Tume ya Haki za Binadadamu na Utawala Bora Tanzania leo imezindua utaratibu mpya wa uwasilishaji wa malalamiko  na taarifa kuhusu uvunjwaji wa wa haki za binadamu  na ukiukwaji wa wa misingi ya Utawala bora kwa njia ya ujumbe wa simu ya kiganjani katika visiwa vya Zanzibar.
Akizindua mfumo huo katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa  Mbweni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar, Kamishna Mkaazi wa  Tume hiyo  Zahor Juma Khamis amesema lengo la mpango huo ni kuboresha utoaji huduma kwa umma.
Amesema utaratibu huo unatarajia  kupunguza usumbufu na gharama kwa walalamikaji hasa wanaoishi maeneo ya mbali katika kuwasilisha malalamiko yao katika ofisi za Tume na kupata marejesho haraka.
“Itakumbukwa kuwa hapo awali baadhi ya wananchi walilazimika kuacha shughuli zao za kiuchumi na kusafiri hadi zilipo Ofisi za Tume ili kupata huduma hiyo, ”alisema Kamishna  Mkaazi Zanzibar.
Ameongeza kuwa utaratibu huo utaharakisha mawasiliano kati ya Tume na walalamikaji kwa upande mmoja na  kati ya Tume na walalamikiwa, kinyume na utaratibu wa awali wa kutumia barua kupitia Posta ambayo ilikuwa ikichukua muda mrefu na kukabiliana na changamoto nyingi ikiwemo kupotea njiani.
Amesema  kupitia mfumo huo mtu anaweza kufungua malalamiko Tume pale ambapo ataona haki zake za msingi zimevunjwa au misingi ya Utawala Bora imekiukwa kwa kuandika ujumbe mfupi wa simu ya kiganjani kwenda namba 0754460259 na atapata majibu kwa muda mfupi.
“Utaratibu huu mpya sio tu unampa uhakika mlalamikaji wa lalamiko lake kufika mbele ya Tume, bali pia unamuwezesha kupata ushauri juu ya lalamiko lake ndani ya muda mfupi, ”alisisitiza  Zahor Juma Khamis.

Ameongeza  kuwa utaratibu huo utaongeza idadi ya malalamiko yanayowasilishwa Tume kutoka wastani wa malalamiko mawili hivi sasa hadi 30 kwa mwezi na tayari wamejipanga kikamilifu kuyashughulikia malalamiko yote ndani ya muda mfupi.
Kamishna Zahor amesema  kwa vile Tume inatambua kuwa wananchi wengi hawana uelewa wa kutuma malalamiko kwa njia ya ujumbe wa simu ya kiganjani hivyo imeandaa mkakati wa kutoa elimu Tanzania nzima kuanzia mwezi ujao ili uweze kueleweka kwa wananchi wote.
Awali Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Bi. Mary Massay amewataka wananchi hasa wanaoishi mbali na Ofisi za Tume kuitumia nafasi hiyo kutuma SMS ya malalamiko yao na hakuna malipo yeyote.
Amesema walengwa wakubwa wa mpango huo ni wananchi wanaoishi vijijini ambao sio rahisi kuzifikia Tume kuwasilisha malalamiko yao.
Utaratibu wa upokeaji wa taarifa na malalamiko kwa njia ya ujumbe mfupi wasimu ya kiganjani umefadhiliwa na mpango wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa nchi zinazoendelea (SPIDER) ya nchini Sweden.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>