Madina Issa na Khamisuu Abdallah
MTOTO wa kiume anaekisiwa kuwa na umri wa miaka sita mkaazi wa Bambi, amepigwa na baba yake kwa kitu kizito na kumsababishia maumivu makali.
Akizungumza na waandishi wa habari hizi, Daktari wa kitengo cha mkono kwa mkono cha hospitali kuu ya Mnazimmoja, Salum Omar Mbarouk, alithibitisha kumpokea mtoto huyo na kusema dalili zinaonesha alivunjika.
Alisema baada ya kumpokea alimpima na kugundua kuwa mtoto huyo alipigwa na kitu kizito kilichomsababishia kuvunjika.
Aidha alisema mtoto huyo baada ya kupelekwa katika mashine ya kuchunguza mifupa (x-ray) ilionesha mtoto alivunjika na tayari ameshaanza kupatiwa matibabu.
Hivyo alitoa wito kwa wazazi na walezi kuwa makini na watoto wao kwani hao ndio tegemeo la baadae.
Aliitaka jamii inapowaokota watoto kama hao wanaofanyiwa udhalilishaji kuripoti kituo cha polisi ili sheria iweze kuchukua hatua zaidi.
“Baba yake ana tabia ya kumuacha mtoto wake nyumbani ambapo huondoka na mtoto wake wa kike sasa huyu huondoka na kwenda kiambo cha juu kwa ajili ya kucheza lakini akirudi huchezea kipigo,” alisema Mratibu wa wanawake na watoto, Mashavu Ramadhan Abdallah,.
Alisema mtoto huyo alimuona kwa bibi ambae alimuhifadhi baada ya kumuona anapigwa.
Sambamba na hayo Mratibu huyo alisema baba huyo ni mzoefu wa matukio ya udhalilishaji kwani alimtahiri mtoto Gumba kwa kutumia kisu huku dawa ikiwa pombe ya kienyeji.
“Baba yake huyu mtoto anaonesha kuwa ni katili sana kwani alimtahiri kwa kisu na pombe ya kienyeji kufanywa ndio dawa,” alisema.
Alisema kwa sasa baba mzazi wa mtoto huyo yupo chini ya ulinzi katika kituo cha polisi Dunga huku mama yake hajulikani alipo.
Nae mtoto Gumba alisema baba yake huwa anampiga mara kwa mara baada ya kutoka kiamboni kucheza na wenzake.