Na Kadama Malunde, Shinyanga
ASILIMIA kubwa ya watoto wenye ulemavu wa ngozi (albino), wanaolelewa katika kituo cha Buhanghija kilichopo mjini Shinyanga, wametelekezwa na wazazi wao kiasi cha kufikia hatua ya watoto hao kutosherehekea sikukuu ya pasaka.
Hayo yameelezwa na mwalimu mlezi wa kituo hicho, Maisala Adinani, wakati familia ya Anna Mwalongo ya mjini Shinyanga, ilipotoa msaada wa chakula kwa watoto hao kwa ajili ya kusherehekea sikukuu ya pasaka.
Alisema baadhi ya watoto wanaolelewa katika kituo hicho wakiwemo wasiosikia na wasioona, tayari wamechukuliwa na wazazi na walezi wao kwenda kusherehekea sikukuu ya pasaka lakini kwa upande wa watoto wenye ulemavu wa ngozi, hakuna mzazi wala mlezi yeyote aliekwenda kuwatembelea wala kuwachukua watoto hao.
Alisema wakati wa sikukuu baadhi ya watoto wenye ulemavu huchukuliwa na wazazi wao,kama walivyofanya kipindi hiki lakini watoto wenye ulemavu wa ngozi hubaki katika kituo hicho siku zote.
Nayo familia ya Mwalongo iliyotoa msaada wa chakula kwa watoto hao, imeelezea kuguswa na watoto hao wanaoishi katika mazingira magumu na kuongeza kuwa iliona si vyema kusherehekea sikukuu ya pasaka peke yao na kuamua kuwatembela watoto hao.
Anna Mwalongo na Josephat Mwalongo ambao ni wanafamilia, walisema jamii inapaswa kutambua kuwa watoto hao ni wa wote na sio kukiachia kituo hicho kila kitu.
“Tumeona ni vyema kuwatembelea na kuwasaidia chakula watoto hawa pamoja na kambi ya kulelea wazee wasiojiweza ya Kolandoto iliyopo mjini Shinyanga, ili wasione kuwa jamii imewatenga kama walivyoachwa na wazazi wao,” walisema.
Familia hiyo haikuishia kutoa msaada katika kituo hicho tu, pia ilitoa msaada katika kambi ya wazee ya Kolandoto.