Na Mwandishi wetu
RAIS Jakaya Mrisho Kikwete, amefanya mazungumzo na majadiliano ya kina na viongozi wa vyama vyote vya wafanyakazi nchini yenye nia ya kutafuta njia za kuboresha maslahi na ustawi wa wafanyakazi.
Mazungumzo hayo ya muda mrefu yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam yalihudhuriwa pia na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi), Celina Kombani, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.
Aidha, mazungumzo hayo yalihudhuriwa na maofisa waandamizi wa serikali wakiwemo Makatibu wakuu wa wizara ambazo zinahusika moja kwa moja na maslahi na ustawi wa wafanyakazi na uongozi wa vyama vya wafanyakazi uliongozwa na uongozi wa juu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).
Rais Kikwete na viongozi hao kwa zaidi ya saa 10 walijadili hali ya utekelezaji wa masuala na mambo yaliyokubaliwa katika kikao chao cha namna hiyo kilichofanyika Februari 27, 2013.
Iidha Rais Kikwete na viongozi hao wakiwemo wale wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) walichambua kwa kina hoja za wafanyakazi zilizowasilishwa kwa Ikulu na vyama hivyo.
Miongoni mwa hoja hizo ni ajira kwa wageni na athari zake kwa ajira ya Watanzania, athari za kuzuka kwa mawakala wa ajira, watumishi waandamizi wa serikali kushikilia nafasi za uongozi katika vyama vya wafanyakazi na athari zake, ushirikishwaji wa wafanyakazi katika bodi za taasisi za umma na serikali na uhamisho wa maofisa kazi ambao Rais Kikwete aliuagiza miaka mitatu iliyopita.
Hoja nyingine zilizojadiliwa ni hali ya afya ya wafanyakazi katika migodi nchini, bei ya umeme majumbani na athari yake kwa wafanyakazi, uwezekano wa kupunguza tena kodi kwenye mishahara ya wafanyakazi jambo ambalo serikali ililifanya mwaka 2013, madai ya malimbikizo ya mapato ya wafanyakazi, madeni ya walimu na uwezekano wa nyongeza ya mishahara kwa walimu.
Katika kikao hicho, Rais Kikwete aliagiza wizara, idara na taasisi zote za serikali na umma ambazo hazijatekeleza mahitaji ya kisheria ya kuundwa kwa mabaraza ya wafanyakazi katika utumishi wa umma kufanya hivyo mara moja bila kuchelewa.
Alitoa muda hadi Mei mosi mwaka huu kwa wizara, idara na taasisi hizo kuwa tayari zimeunda mabaraza hayo na alimwagiza Balozi Sefue kutuma barua za maagizo ya Rais kwa wizara, idara na taasisi inayohusika.
Aidha alisema mwishoni mwa mwaka huu, atapenda kupata taarifa kuhusu hali ya uanzishwaji na utendaji wa mabaraza hayo ambayo ni muhimu kwa uwakilishi wa wafanyakazi katika uendeshaji wa taasisi za umma ambazo wanazifanyia kazi.