Na Kadama Malunde, ITILIMA
WAZIRI Mkuu (mstaafu) Edward Lowasa, ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya mwanasiasa maarufu nchini ambaye pia ni Mbunge wa zamani wa Bariadi kupitia CCM, Edward Masanja Ng’wani aliyefariki dunia hivi karibuni.
Marehemu ambaye ni miongoni mwa waasisi wa CCM amefariki dunia Aprili 13 wakati akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa saratani ya kibofu cha mkojo katika hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam.
Akitoa salamu hizo kwa niaba ya Lowasa, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, alisema CCM imepoteza kiongozi shupavu ambaye mchango wake ulikuwa bado unahitajika.
Katika salamu zake kwa familia ya marehemu, Lowasa alisema alimfahamu marehemu kwa miaka zaidi ya 35 iliyopita ambapo alifanya naye kazi za uongozi katika mkoa wa Shinyanga wakati Lowasa akiwa Katibu msaidizi wa CCM mkoa huo.
“Ng’wani alikuwa mwanachama na mwanasiasa mwaminifu, mkweli na jasiri katika kutetea wananchi, hakika familia na wanaCCM mkoa wa Simiyu na kanda ya ziwa wameondokewa na kiongozi shupavu,” alisema Lowasa katika salamu zake.
Aidha alisema CCM itaendelea kukumbuka mchango wa marehemu kimawazo na ushauri wake ndani ya chama na jamii kwa ujumla huku akiwataka wananchi kuendelea kumwombea kwani chama na wanajamii walimpenda lakini mungu kampenda zaidi.
Aliiomba familia ya marehemu kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba.
Marehemu Ng’wani alizaliwa 1935 katika kijiji cha Bunamhala katika wilaya ya Itilima mkoa mpya wa Simiyu na mazishi yake yamefanyika katika kijiji alichozaliwa Aprili 18.