Na Donald Martin
ASKOFU wa jimbo Katoliki la Zanzibar, Augustino Shao, ameyataka makundi yanayokinzana katika bunge maalum la katiba, kuachana na ubinafsi na itikadi za kisiasa ili kufikia muafaka katika masuala muhimu.
Askofu Shao alitoa rai hiyo katika ujumbe wa sikukuu ya Pasaka kwenye ibada ya misa ya mkesha wa sikukuu hiyo, iliyofanyika katika kanisa la Minara miwili mjini Zanzibar .
"Sasa tunashuhudia makundi yenye nguvu yakijaribu kushinikiza kuingizwa matakwa yao kwenye katiba kwa njia zozote ili kuendelea kulinda maslahi yao ya kisiasa," alisema.
Aliwataka wajumbe wa bunge hilo kufanya kazi kwa uadilifu ili kufikia muafaka katika masuala muhimu yatakayowahakikishia raia wa kawaida kushiriki kwenye fursa za maendeleo kwa manufaa ya wote.
Alisema ili kupata katiba bora hakuna kuiheshimu kazi ya Tume ya Mabadliko ya Katiba pamoja na kuwa na nia njema ya kutafuta suluhisho la matatizo mengi ya utendaji katika dola zilizopo katika Muungano.
"Chaguo la muundo wa dola sharti liongozwe na malengo na madhumuni ya umoja wetu wa kutaka tuishi kwa mshikamano. Muundo wa serikal moja, mbili au tatu sharti ufanywe kwa dhamira safi ya kupata suluhisho la matatizo ya Muungano," alisema.
Aliwapongeza Rais Kikwete na Rais Shein kwa ujasiri wa kuamua kuanzisha mchakato wa kuandika katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kisheria na katika wakati muafaka.
Wakati huo huo, Francis Godwin kutoka Iringa anaripoti kuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Kilutheri (KKT) Dayosisi ya Iringa, Dk. Owdenburg Mdegela, amelaani vikali wale wote wanaowatukana waasisi wa taifa, marehemu Sheikh Abeid Amani Karume na hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Akizungumza katika misa ya Pasaka, alisema watu hao wanapaswa kuwaomba radhi Watanzania huku akisisitiza wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kurejea bungeni au wafungashe virago na kurudi nyumbani.
Askofu huyo ambae pia ni mjumbe wa bunge maalum la katiba, alisema Watanzania wanataka kuikataa lulu waliyopewa na Mungu lulu ya amani na kuanza kutafuta kuvurugana.
"Kinachofanywa bungeni kwa sasa ni mzaha wa hali ya juu na Watanzania wanapaswa kuwachunguza vyema wawakilishi wao hao wakiwemo wabunge wa vyama vyote na wale wanaoeneza mbegu ya chuki,” alisema.
Asema wajumbe wa bunge la katiba hawana sifa ya kutengeneza katiba kwani wametanguliza mzaha na matusi yasiyo na tija na kwamba wanaokwepa bunge na kutaka kuzunguka kwa wananchi wanapaswa kuzuiwa na vyombo vya usalama .
"Kama wamekula pesa za wananchi kwa muda wote huo kwa ajili ya kuunda katiba iweje leo watoke bungeni na kudai kwenda kwa wananchi mikono mitupu,” alihoji.
"Wananchi tuwakatae wajumbe wanaotaka kuzunguka kupandikiza chuki kwa kujiita wao wapo kwa ajili ya katiba ya wananchi ilhali wamekimbia bunge na kutaka kutuwakilisha nje ya bunge,” alisema.
Aliwataka Watanzania kuyatazama mataifa jirani kama Kenya ambao walijipenda wao na kushindwa kuwapenda majirani sasa Wasomali wameingia wanawasumbua.
Nae Jumbe Ismailly kutoka Singida, ameripoti kwamba Askofu wa Kanisa la Miracle Assemblies of God Ministry la mjini Singida, John Tesha, ametoa wito kwa Watanzania kuchunga kauli zao wanazotoa katika kipindi hiki ambapo wajumbe wa bunge maalumu la katiba wanaendelea na mchakato wa kujadili rasimu ya katiba.
Alitoa wito huo kwenye hafla ya uzinduzi wa kanisa la Miracle Assembles of God Ministry pamoja na kuwekwa wakfu kuwa Askofu wa kanisa hilo, iliyokwenda sambamba na harambee ya kuchangia ujenzi wa skuli ya maandalizi ya kanisa hilo .
“Mimi nataka kutoa rai tu kwa Watanzania wote na siyo kwa wale waliopo Bungeni pekee kuwa wajaribu kuelewa kwamba maneno mengi siyo sababu ya kujenga nchi, bali wanatakiwa wachukulie neno la upendo ili kujenga umoja,” alisema.
Alisema kwa muda mrefu Watanzania wamekuwa wakiishi katika hali ya amani, utulivu, upendo na mshikamano kwa hivyo kanisa halitakuwa tayari kuona Watanzania wakivurugana,” alisema.
“Unajua chuki inapopandwa katikati ya jamii inaleta kufarakanisha watu lakini sisi tunataka watu wapendane na wawe na amani ili tuendelee kujenga taifa bora,” alisema.
Kwa upande wake Waziri wa Mali Asili na Utalii, Lazaro Nyalandu ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, aliwaomba maaskofu na wachungaji kuongeza kasi ya kuwahubiria waumini wao ili waweze kuona faida ya kuchangia katika masuala ya dini zao.