Na Mwandishi wetu
RAIS Jakaya Mrisho Kikwete, amekabidhi vitabu 2,181 kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa ajili ya vyuo vya jeshi ili kuongeza taaluma.
Rais alikabidhi vitabu hivyo kwa Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange na kuahidi kuendelea kutafuta vitabu zaidi kwa ajili ya kuboresha maktaba ya jeshi iliyopo katika Chuo Cha kijeshi kilichopo Monduli, Mkoani Arusha.
Maktaba hiyo ilianzishwa na Rais Kikwete wakati alipokuwa mkufunzi katika chuo hicho miaka iliyopita.
"Lazima mtenge bajeti kwa ajili ya vitabu lakini na mimi nitaendelea kutafuta vitabu niwaletee ili kuijengea uwezo maktaba yetu ya Monduli,” alisema.
Akipokea vitabu hivyo kwa niaba ya Jeshi, Jenerali Mwamunyange alimshukuru Rais kwa juhudi zake za kuboresha JWTZ kwa ujumla na kulifanya kuwa la kisasa zaidi.
“Juhudi zako za kuliendeleza jeshi letu imetuongezea uwezo na kujiamini zaidi. Bila juhudi zako tusingefika hapa tulipo na tunajivunia mafanikio haya,”alisema Jenerali Mwamunyange.