Na Masanja Mabula, Pemba
Tatizo la akina baba kutoshiriki kikamilifu katika suala la chanjo kwa kufuatana na akinamama kuwapeleka watoto kliniki kwa ajili kupatiwa chanjo, limedaiwa kuwa moja ya sababu zinazozorotesha ufanisi wa zoezi hilo .
Ofisa Tawala wilaya ya Wete, Mwalimu Khamis Juma Silima, aliyasema hayo wakati akizindua wiki ya chanjo barani Afrika ambayo kwa wilaya ya Wete yaliadhimishwa katika kituo cha afya Kiungoni.
Aliwataka akinababa kusimamia suala la chanjo kwa kuhakikisha wanaambatana na akinamama kuwapeleka watoto kupatiwa chanjo katika vituo vya afya.
Katika hotuba iliyosomwa kwa niamba yake na Ofisa Utumishi Wilaya hiyo, Abdalla Ali Nuhu, Ofisa Tawala, alisema suala la kuwapeleka watoto kupatiwa chanjo linawahusu wazazi wote katika familia.
Alisema baadhi ya akinababa wamekuwa wakiwaachia jukumu la kuwapeleka kliniki watoto akinamama hali ambayo inakwamisha kupatikana ufanisi.
"Akinababa nao wanajukumu la kufuatana na akinama kuwapeleka watoto kupatiwa chanjo, kwani kwa sasa bado wapo baadhi ya akinababa wanashindwa kutambua kuwa kufanya ni hivyo ni wajibu wao kama wazazi,” alisema.
Aidha, alisema ni vyema wananchi wakaitumia vyema fursa ya maadhimisho ya wiki ya chanjo Afrika kwa kuhakikisha watoto wanaostahiki kupata chanjo hizo wanapatiwa kwa wakati.
Naye Ofisa wa afya wilaya hiyo, Dk. Ali Rashid Said, ameitaka jamii kuondoa dhana kwamba chanjo hizo zinapunguza uzazi kwa watoto.
Alisema serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kwa ajili ya kutoa huduma za chanjo kwa wananchi wake, hivyo ni vyema wakajitokeza kwa ajili ya kuwachanja watoto wao.
Wiki ya chanjo Afrika huadhimishwa kila ifikapo wiki ya mwisho wa mwezi Aprili kila mwaka ambapo Mkuu wa kituo cha afya Kiungoni, Dk.Hamad Khamis, aliwataka wazazi kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo .