Na Mwashamba Juma
Jumla ya vijana 1,034 wakiwemo wanaume 692 na wanawake 342 kutoka makundi maalum, wamejitokeza kupima virusi vya UKIMWI kwa kipindi cha miezi sita.
Kati ya vijana hao, 775 ambapo wanaume 516 na wanawake 259 kutoka makundi ya kakapoa (MSM), wafanyabiashara za ngono, watumiaji wa dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga sindano (IDU) pamoja na wagonjwa wa kifua kikuu walipimwa.
Akitoa takwimu hizo kwa mujibu wa ripoti ya UNICEF ya mwezi Oktoba-2013 hadi Machi mwaka huu, katika mkutano maalum ulioushirikisha mtandao wa wadau wa kupambana na ugonjwa wa UKIMWI Zanzibar (CSOs) na makundi maalum katika ukumbi wa kituo cha huduma rafiki cha ZAYEDESA, Miembeni mjini Unguja, Ofisa takwimu wa ZAYEDESA, Jackson Joseph, alisema watu 17 wakiwemo wanawake kumi na moja na wanaume sita waligunduliwa kuambukizwa virusi vinavyosababisha UKIMWI.
Alisema kati ya watu hao 10 wamejiunga na vituo vya afya vilivyopo hospitali ya Mnazi Mmoja, Bububu na Mwembeladu.
Aidha alisema vijana 125 wakiwemo wanawake 64 na wanaume 61 walipimwa maradhi ya kujamiiana (STI) na 27 miongoni mwao wanaume 14 na wanawake 13 walipimwa TB ambapo kesi mbili zilipatikana.
Akizungumzia changamoto na mafanuikio ya miradi ya UNICEF katika mkutano huo, Mratibu wa ZAYEDESA, Mgoli Mgoli, alisema tatizo ni kupima aina moja ya kundi la kaka poa (MSM) pasi na wahusika wengine ambao ni wafanyaji kutojitokeza kupima UKIMWI na badala yake hujitokeza wafanywaji pekee.
“Wanaojitokeza kupimwa ni kundi la upande mmoja na sio marafiki, tumefanya jitihada za kuwafikia ingawa ni vigumu kujitokeza na kujitambulisha kuwa ndio wahusika,” alisema.
Nae Mratibu wa makundi maalum na maradhi ya kujamiiana kutoka Wizara ya Afya,k itengo cha UKIMWI Zanzibar, Dk. Shaaban Hassan Haji ambae pia ni rais wa mtandao wa (CSOs), alisema ni vigumu kwa kundi la wafanyaji (MSM) kujitokeza kupima VVU kwani baadhi yao ni watu wenye taaluma na vyeo vikubwa vya uongozi katika serikali na badala yake alishauri kupewa elimu juu ya maambukizi ya UKIMWI kwa kundi la wafanywaji.
Kwa upande wa washiriki wa mkutano huo, walisema tatizo la mtu mmoja kupima zaidi ya mara moja ni changamoto inayozikumba taasisi zao, hivyo ni vigumu kwao na serikali kuwadhibiti.
Aidha, waliwashauri wanandoa watarajiwa kupima kabla ya kufunga ndoa sambamba na kupokea matokea kwa pamoja ili kuepusha udanganyifu baina yao na kujikinga na maambukizi ya UKIMWI.
Hata hivyo, walipendekeza kuwa na mawasiliano ya pamoja kwa lengo la kubadilishana uzoefu sambamba na kuisaidia jamii kupata taarifa za haraka na zilizo sahihi.
Wakati huo huo, Meneja Miradi wa ZAYEDESA, Aisha Ali Karume, alisema taasisi yake imefanikiwa kupambana na unyanyapaa kwa kutoa taaluma kwa jamii pamoja na kuwashirikisha viongozi wa serikali kwa kuzungumza nao.