Na Haji Nassor, Pemba
Baada ya kampuni ya MECCO kusimamisha ujenzi wa barabara za Gando na Konde kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu, sasa ujenzi huo umenza tena, kwa matengenezo ya sehemu zilioathirika, baada ya kukabidhiwa zaidi ya shilingi bilioni tano.
Awali ujenzi wa barabara hizo, ulianza tokea mwaka 2009 na kampuni hiyo kusitisha ujenzi wake kutokana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na washirika wake Benki ya Maendeleo ya Afrika pamoja na Mfuko wa Saudi Arabia, kutoingiza fedha kwa wakati.
Uchunguzi umebaini mara baada ya kusaiini mkataba wa ujenzi wa barabara hizo, kampuni ya MECCO ilianza ujenzi Septemba 1, 2009 na ilitakiwa kukamilisha ujenzi wa barabara hizo kwa kiwango cha lami, Januari 1, 2012.
Hata hivyo, kazi hiyo ilishindikana kutokana na kujitokeza mambo kadhaa na baadae kampuni hiyo iliomba kuongezewa miezi nane zaidi, ambapo iliahidi kumaliza ujenzi huo Agosti 27, 2012 ingawa pia haikumaliza.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia simu, Ofisa Mdhamini wa wizara hiyo, Hamad Ahmed Baucha, alikiri kwamba kwa sasa ujenzi huo umeanza na utaendelea moja kwa moja hadi kukamilika kwa kiwango cha lami.
Alisema ujenzi wa barabara ya Wete- Gando na Wete-Konde umeanza hasa katika maeneo yaliyoharibika kutokana na kukatika kwa mvua.
Alisema hivi karibuni MECCO, ilishakabidhiwa shilingi bilioni tatu kwa mara ya kwanza na mara ya pili hakumbuki ni kiasi gani ilipewa lakini jumla ni zaidi ya shilingi bilioni tano.
Mhandishi kutoka wizara ya Miundombinu na Mawasiliano anaefuatilia ujenzi huyo, Rashid Issa Rashid, alisema kwa sasa ujenzi huo umeanza taratibu na ana matumanini kwamba, utaendelea hadi kumalizia kwa kiwango cha lami.
“Nilisikia kwamba MECCO wameshatimiziwa madai yao ya fedha, hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi na waondoe hofu, kwani wizara kwa kushirikiana na washirika wake wa maendeleo, inayo nia thabiti ya kuwatandikia wananchi lami,’’alisema.
Katika hatua nyengine, Ofisa Mdhamini huyo alisema hakuna hata nyumba moja iliovunjwa wakati huo wa ujenzi na ambayo mmiliki wake hajalipwa fidia.
Alibainisha kuwa kilichobakia ambacho hakijalipwa ni zile nyumba zilizoharibika wakati wa ujenzi pamoja na fidia kwa miti iliyokatwa na vipando vilivyoharibika.
Aliwataka wananchi wa maeneo mbalimbali kuendelea kuwa wastahamilivu na serikali kamwe haijasahau kuwapa haki zao.
Baadhi ya wananchi wanaotumia barabara hizo walisema pamoja kwamba kampuni imeanza kazi, bado hawana hakika kwamba barabara zao zitamalizika kwa kiwango cha lami kutoka na kampuni hiyo kufanya kazi kwa kusua sua.
Kampuni ya ujezi wa barabara ya MECCO ilianza ujenzi wa barabara za Wete–Gando na Wete–Konde zenye urefu wa kilomita 30, mwaka 2009 na ikitarajiwa kukabidhi kwa serikali Januari 1, mwaka 2012.