Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Wazanzibari 12 washikiliwa Madagascar

$
0
0
Na Kauthar Abdalla
WAZANZIBARI 12 wanashikiliwa na vyombo vya usalama katika kisiwa cha Madagascar kwa tuhuma za kuingia nchini humo kwa njia ya haramu.

Watu hao ambao ni nahodha pamoja na mabaharia 11 wanaofanyakazi katika meli ya mizigo ya MV Wete inayomilikiwa na mfanyabiashara maarufu visiwani Zanzibar, Saidi Mbuzi, wanashikiliwa nchini humo baada ya meli hiyo kupata  hitilafu za kiufundi wakati ikiwa njiani kuelekea katika kisiwa cha Mauritius.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, baadhi ya ndugu na jamaa wa watu hao, walisema baada ya kuharibika meli hiyo ambayo ilikuwa imebeba mizigo, nahodha aliamua kutia nanga katika visiwa vya Madagascar kwa ajili ya matengenezo.
Walisema wakati wakiendelea na matengenezo walivamiwa na maofisa wa usalama wa Madagascar na kuwakamata kwa kuingia nchini humo kinyume cha sheria.

Kwa mujibu wa taarifa za ndugu zao, wananchi hao walisema meli hiyo iliondoka Zanzibar tokea Februari 2 mwaka huu kuelekea Mauritius.


Mmoja ya watu hao aliyejitambulisha kwa jina la Fatma Hassan Khamis ambae ni mke wa nahodha wa meli hiyo aliemtaja kwa jina la Amour Ali Juma, alisema alipigiwa simu na mumewe na kumuarifu kuwa wanashikiliwa nchini Madagascar baada ya meli yao kupata hitilafu.

Mwengine Mohammed Ali Haji ambae ndugu yake, Haji Ali Haji anashikiliwa huko, alisema nduguye alimwambia kuwa wametakiwa kulipa fidia yenye thamani ya shilingi milioni 17 za Tanzania, ili waachiwe huru lakini fedha hizo hawana.

Aidha, walisema wamechukua juhudi za kumfuata mmiliki wa meli hiyo kuzungumzia sakata hilo, lakini hadi sasa hawajampata.

Ofisa kutoka Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) ambae alikataa kutaja jina lake kwa kuwa sio msemaji wa mamlaka, alisema hakuna taarifa rasmi zilizofikishwa na mmiliki wa meli hiyo kuhusu sakata hilo.

Nae mmiliki wa meli hiyo katika mazungumzo kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hizi, alikiri meli hiyo pamoja na mabaharia wake kukamatwa nchini Madagascar, lakini akasema kuwa suala hiloamelifikisha serikalini ili kuchukua hatua.

Kuhusu kufuatwa na ndugu za mabaharia hao, aliwataka kuendelea na subra wakati serikali ikiendelea kuchukua hatua ili kuhakikisha ndugu zao wanaachiwa huru.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>