Na Haji Nassor, Pemba
Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kisiwani Pemba, imekiri kupokea barua ya kutaka ufafanuzi wa kisheria, kutoka kwa ndugu na jamaa wa marehemu Omar Bakar Omar, alieuawa akiwa mikononi mwa polisi, wakidai wamegundua mchezo mchafu juu ya tukio hilo .
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mdhamini wa ofisi hiyo kisiwani humo, Albaghiri Yakuot Juma, alisema awali kabla ya kupokea barua hiyo, wawakilishi wa familia ya marehumu, walifika ofisini kuomba utaratibu wa kuandika barua hiyo.
Alisema baada ya kuwaelekeza kwa kina, hatimae wiki mbili zilizopita waliwasilisha barua hiyo, inayolilalamikia jeshi la polisi mkoa wa kaskazini Pemba, kwa kushindwa kuchukua hatua baada ya kutokea mauaji ya ndugu yao .
Alisema baada ya wao kuipokea barua hiyo, amemkabidhi mwanasheria wao kwa hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na kufuatilia kwa Mkuu wa upelezi wa makosa ya jinai mkoani humo, ili kujua hatua ya uchunguuzi ulipofikia.
Alisema baada ya hapo, yeye binasfisi aliwasiliana na RCO huyo ingawa alimpa majibu kwamba ndio kwanza anaripoti kazi, hivyo ni vyema akampa nafasi ili kulifuatilia kwa kina suala hilo .
Katika hatua nyengine, aliwaomba ndugu na jamaa wa marehemu kufuatilia suala hilo kila mara kwa vile ofisi hiyo haina kazi moja.
Mmoja wa ndugu wa marehemu, Salim Bakari Omar, alisema ni kweli baada ya kuona jeshi la polisi limewatelekeza juu ya tukio hilo, waliamua kwenda kwa DPP kufuata utaratibu wa kisheria.
“Tokea mwezi Machi kaka yetu alipopigwa risasi na polisi wa mkoa wa kaskazini Pemba, hali imebaki kuwa shwari kama alieuawa alikuwa kuku, hata hatujaulizwa lolote, ndio maana tukaenda ofisi ya DPP kwa hatua za kisheria,” alisema.
Hivyo, alisema watahakikisha suala hilo, linafikia kikomo cha kisheria na kuviomba vyombo vinavyohusika kuhakikisha wanawasaidia, kutokana na kukumbwa na msiba mzito wa kaka yao .
Kamanda wa polisi mkoa wa kaskazini Pemba, Sheikhan Mohamed Sheikhan, alisema jeshi la polisi mkoani humo, haijaitelekeza familia ya marehemu, ingawa uchunguzi wa suala hilo umefanywa makao makuu ya polisi Unguja.
Alisema makao makuu ndio itatoa majibu juu ya tukio hilo lililotokea Machi 19 mwaka huu na hapo ndipo atajulikana nani sheria imchukulie hatua.
Alipopigiwa simu DCI Ilembo juu ya hatua ya uchunguuzi ulipofikia, alisema hakuna anaepaswa kujua lolote kutokana na kazi anayoifanya yeye na tume yake.
Alimwambia mwandishi wa habari hizi, kwamba taarifa za tume yake hazimuhusu huku akisisitiza kuwa hawezi kusema tume inaweza kumaliza uchunguzi wa tukio hilo muda gani.
“Sasa wewe mwandishi umesikia wapi kwamba uchunguzi unawekewa siku, nnanvyokueleza mimi sina cha kukwambia juu ya tukio hili maana bado uchunguzi unaendelea na sijui lini utamaliza”, alisema kwa ukali Ilembo.
Hata hivyo, baada ya kukata simu baadae alimpigia simu mwandishi wa habari hizi, akamwambia kuwa upelelezi wa tukio unaendelea.
Uchunguzi wa awali uliofanywa na mwandishi wa habari, umebaini kuwa jalada la kesi hiyo tayari limeshafikishwa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Unguja, ingawa juhudi za kumpata Mkurugenzi hazikuzaa matunda.
Machi 19 mwaka huu, majira ya saa 3:00 usiku, eneo la Bahanasa shehia ya Piki wilaya ya Wete, kuliripotiwa kuuawa kwa mzee Omar Bakar Omar (54), baada ya kupigwa risasi ya ubavuni na polisi waliokuwa doria, baada ya kudaiwa kutaka kuwavamia polisi, madai ambao yalikanushwa na wanafamilia.