Na Madina Issa
Serekali ya Mapinduzi ya Zanzibra na Kampuni ya Don Consult ya Dar es Salaam,zimetiliana saini mkataba wa mradi wa maji safi na salama pamoja na usafi wa mazingira mjini Zanzibar (ZUWSSP) hususani maeneo ya Mji Mkongwe.
Akisaini msaada huo katika hoteli ya Bwawani, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), Dk. Mustafa Ali Garu na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Laurent Mzee Sechuceo, walisema mradi huo utagharimu jumla ya dola za Marekani milioni 21 zikiwa ni sawa na shilingi bilioni 34.
Mradi huo utaimarisha huduma ya maji katika maeneo ya mjini Unguja hususani Mji Mkongwe na maeneo jirani pamoja na kuijengea uwezo ZAWA ili iweze kumudu vyema kazi zake.
Dk. Garu alisema mradi huo una lengo la kusaidia uimarishaji huduma za maji katika maeneo hayo pamoja na kukarabati mabomba ambayo yameshachakaa.
Aidha kutokana na kukua kwa mji wa Unguja, kumesababisha mahitaji ya maji kuongezeka, hivyo ZAWA inachukua juhudi kuhakikisha kila mtu anafaidika na huduma ya maji
Alisema mradi huo utatekelezwa katika kipindi cha miaka minne na umeanza mwaka jana na unatarajia kukamilika 2016 na kuwanufaisha wakaazi wote wa shehia za Mji Mkongwe pamoja na baadhi ya wanafunzi kadhaa ambao watapatiwa huduma za vyoo katika skuli zao.
Aliwaomba wadau wote zikiwemo taasisi za serikali na binafsi, masheha na wakaazi wa maeneo jirani ya mradi huo, kushirikiana kwa pamoja na mamlaka ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa.
Nae Mkurugenzi wa kampuni ya Don Consult, Laurent Mzee Sechuceo, alisema mradi huo watausimamia kwa kiwango kikubwa ili kuhakikisha wananchi wa mji Mkongwe wanapata huduma ya maji.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na watendaji mbalimbali wa serikali akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Zanzibar, Mustafa Aboud Jumbe, Masheha wa Mji Mkongwe, viongozi wa mipango miji wa mji Mkongwe pamoja na viongozi Jumuiya ya Uhifadhi wa Mji Mkongwe.