Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza kwenye Kikao cha Utiaji saini makubaliano maalum kati ya Mradi wa Hoteli ya Sea Cliff na Uongozi wa Kamati Nne za Vijiji vya Kiomba Mvua.
Baadhi ya watendaji wa Taasisi mbali mbali za Serikali walishiriki vikao vya usuluhishi wa mzozo wa ardhi kati ya Mradi wa SEA Cliff na Wananchi wanaouzunguuka mradi huo.
Baadhi ya Viongozi wa Mradi wa Hoteli ya Kimataifa walioshiriki vikao vyote vya kutafuta suluhu ya matumizi ya ardhi kati yao na Wananchi wa jirani na Mradi huo.
Hata hivyo Viongozi wa Kamati za Wana Vijiji hao hawakufika kwenye kikao hicho licha ya kushiriki hadi hatua ya mwisho na kuridhia kwa pamoja makubaliano yaliyofikia hatua ya kutiwa saini hiyo.
Kulia ya Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mh. Pembe Juma Khamis na kushoto yake ni Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini : B” Nd. Khamis Jabir.
Baadhi ya watendaji wa Taasisi mbali mbali za Serikali walishiriki vikao vya usuluhishi wa mzozo wa ardhi kati ya Mradi wa SEA Cliff na Wananchi wanaouzunguuka mradi huo.
Baadhi ya Viongozi wa Mradi wa Hoteli ya Kimataifa walioshiriki vikao vyote vya kutafuta suluhu ya matumizi ya ardhi kati yao na Wananchi wa jirani na Mradi huo.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameuagiza Uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Kaskazini Unguja pamoja na Wilaya ya Kaskazini “B” kusimamia ipasavyo makubaliano yaliyofikiwa kati ya Muwekezaji wa Hoteli ya Kimataifa ya Sea Cliff iliyopo katika Kijiji cha Kama na Wananchi wa Vijiji vinavyoizunguuka Hoteli hiyo.
Amesema makubaliano hayo yalifikiwa na pande hizo mbili kufutia Vikao mbali mbali vilivyokuwa vikiendelea vya kutafuta maridhiano ambapo yeye binafsi alikuwa shahidi wa vikao hivyo.
Balozi Seif alitoa agizo hilo hapo katika Ukumbi wa Hoteli ya Sea cliff wakati wa kikao maalum kilichotayarishwa kwa ajili ya utiaji saini wa makubaliano ya pande hizo mbili lakini chakusikitisha wale wawakilishi wa kamati husika na makubaliano hayo hawakuhudhuria licha ya kupata taarifa kamili ya kikao hicho.
Alisema makubaliano ya pande hizo mbili bado yataendelea kuwa halali kwa vile vikao vyake vilishirikisha wajumbe na Viongozi wa pande zote zinazohusika ukiwemo uongozi wa Serikali wa Mkoa wa Kaskazini Unguja pamoja na ule wa Wilaya ya Kaskazini “ B”.
Alifahamisha kwamba hali ya mgogoro wa Kiomba mvua ulifikia hatua ya makubaliano mazuri lakini kinachoonekana hivi sasa baadhi ya watu kuanza kuhusisha makubaliano hayo na masuala ya Kisiasa.
“ Mimi nimekuja hapa kama Kiongozi wa Serikali ili kuona namna gani hatma ya pande hizi mbili inafikia pahali pazuri. Kinachoonekana kwa sasa hivi ni baadhi ya watu kujaribu kujitafutia umaarufu kwa mgongo wa Kisiasa “. Alisema Balozi Seif.
“ Wenzetu tuliokuwa nao katika vikao karibu vitatu hii hatua ya mwisho kabisa hawakuja bila ya sababu. Lakini Vikao vya kujadili makubaliano ya muongozo uliotolewa na Kamati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar nao pia walishirikishwa kikamilifu “. Alisisitiza Balozi Seif.
Mapema Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mh. Pembe Juma Khamis alisema Serikali ya Mkoa huo haiwezi kustahamili uchochezi unaoonekana kuanza kupaliliwa na baadhi ya wana siasa kwa kujaribu kuwapotosha Wananchi.
Mh. Pembe alisema juhudi kubwa zimechukuliwa katika kuona kwamba pande hizo mbili zilizokuwa zikizozana inafikia pahali pazuri lakini kinachojitokeza hivi sasa ni kwa baadhi ya wana siasa kuanza tabia ya kushawishi wananchi hao kuyakataa yale makubaliano ambayo tayari wameshayapitia na kuyaridhia.
“ Sisi kama viongozi wa Mkoa na Wilaya tumefikia mwisho wetu kufuatia hatma ya tatizo hilo liloashiria kutaka kuvunjika kwa amani. Kilichobakia hivi sasa ni utekelezaji wa mapendekezo yote yaliyokubaliwa kati ya muwekezaji huyo na Wananchi hao “. Alifafanua Mh. Pembe.
Akitoa ufafanuzi Mkurugenzi wa Ardhi Nd. January Fusi alisema kwamba ni jukumu la Serikali Kuu wakati wote kulinda mali za Wananchi sambamba na zile za Wawekezaji walioamua kuwekeza Vitega Uchumi vyao Nchini.
Nd. Fusi alieleza kwamba Ardhi hivi sasa inaeleweka kuwa ni moja ya cyanzo vikuu vya uchumi wa nchi ambayo hutumiwa katika uwekezaji vitega uchumi mbali mbali ikiwemo sekta ya Utalii inayoonekana kuchukuwa nafasi ya juu katika uchumi wa Dunia.
Naye kwa upande wake Muwakilishi wa Muwekezaji wa Hoteli ya Kimataifa ya Sea Cliff Bwana Yassir De Costa alisema muwekezaji wa mradi huo bado ana nia safi ya kutaka kusaidia maendeleo ya Wananchi kupitia mradi huo wa Utalii.
Bwana De Costa alisema mradi wa Hoteli ya Sea Cliff ambao unalenga kujenga uwanja wa Mchezo wa Golf unatarajiwa kutoa fursa kubwa za ajira na kusisitiza kwamba kipaumbele kitawekwa kwa wananchi walio jirani na mradi huo.
Mwakilishi huyo wa mradi wa Sea Cliff aliiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha kwamba mradi huo unaohusisha watalii wa daraja la juu Duniani kwa nia ya kusaidia kuongeza mapato ya Nchi na wananchi wake unafanikiwa kwa maslahi ya muwekezaji, Serikali pamoja na Wananchi wa Vijiji jirani.
Vikao vya pamoja kati ya Uongozi wa Hoteli ya Sea Cliff na Viongozi wa Kamati Nne za Vijiji vya Kiomba Mvua vilikuwa vikifanyika kwa pamoja kupitia muongozo uliotolewa na Kamati ya Baraza la Wawakilishi kuhusu maridhiano ya pande hizo mbili.
Hivi karibuni Wajumbe wa Kamati hizo Nne walikuwa wakisisitiza ulazima wa kuwepo kwa vikao vya pamoja na muwekezaji huyo ili kujadili mzozo wa ardhi ambayo inatarajiwa kutumika kwa mchezo wa Golf suala ambalo liliridhiwa na muwekezaji huyo na hatimae kufikia makubaliano hayo ambayo wanakamati hao walishindwa kuhitimisha.
Mzozo kati ya Hoteli ya Sea Cliff na Wananchi wa Kiomba Mvua ulikuwa unahusu matumizi ya bandari, eneo la kuanikia madagaa pamoja na Bara bara masuala ambayo yote yamekubaliwa na muwekezaji huyo.
Katika muelekeo wa kusaidia maendeleo ya wananchi wa Kiomba Mvua na Maeneo jirani Mradi wa Hoteli ya Sea Cliff umekubali kuwanunulia mashine ya kuanikia dagaa, kusaidia utunzaji wa mazingira ya Mikoko, Gari ya usafiri, Mabanda ya Wavuvi, na vyoo vyake pamoja na ujenzi wa bara bara.
Hata hivyo Wananchi hao walipendekeza gharama za ununuzi wa mashine hiyo ielekezwe katika kuwaanzishia miradi mipya itakayowasaidi kuongeza kipato chao na kupunguza ukali wa maisha ombi ambalo limeridhiwa na muwekezaji huyo.