Mkuu wa mkoa wa kaskazini pemba Dadi Faki Dadi amewataka wafanyakazi wa sekta ya umma kuheshimu maamuzi ya serikali na kutojiingiza katika migogoro ya kijamii.
Amesema wafanyakazi wa serikali wanapaswa kuwa kioo kusaidia mipango ya serikali na kitendo cha wao kujiingiza katika migogoro ni kwenda kinyume na sheria za uajiri.
Akizungumza na wafanyakazi wa wizara mbalimbali wanaoishi katika shehia ya kambini na mchangamdogo katika kikao cha kusuluhisha mgogoro unaoendelea amesema mgogoro wa kugombania skuli katika shehia hizo unadaiwa kuchangiwa na baadhi ya wafanyakazi wa serikali.
Dadi amesema serikali haiwezi kuwafumbia macho wafanyakazi hao na hatua za kisheria na kinidhamu zitachukuliwa.
Katika hatua nyengine Dadi amemsimamisha kazi sheha wa shehia ya mchangamdogo kutokana na kuhusika kushawishi wananchi kuendeleza mgogoro huo uliosababisha skuli hiyo kufungwa na wanafunzi kukosa masomo.