Na Othman Ame OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati umefika kwa Wanafunzi Nchini kuendelea kujifunza Taaluma mbali mbali kupitia mfumo wa kisasa wa Teknoloji ya Habari na mawasiliano { Teknohama } ili kwenda sambamba na mabadiliko ya Sayansi Ulimwenguni.
Balozi Seif alisema hayo katika hafla fupi ya kukabidhi msaada wa Kompyuta 230 kwa ajili ya Skuli mbali mbali Unguja na Pemba iliyofanyika Makao Makuu ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya amali Mazizini Nje kidogo ya Maji wa Zanzibar.
Msaada huo wa Kompyuta 230 zilizofikishwa hapa Zanzibar ni miongoni mwa Kompyuta 2,500 zilizoahidiwa kutolewa msaada na Rotary Klabu ya Kimataifa inayojishughulisha na Kituo cha uungaji na matengenezo ya Kompyuta katika Mji wa Seattle Nchini Marekani.
Rotary Klabu hiyo ilifikia uamuzi huo wa kutoa msaada kufuatia ziara yake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliyoifanya Seattle Marekani mwishoni mwa mwaka 2013 kuhudhuria Mkutano wa 15 wa Chama cha Wafanyabiashara wenye asili ya Bara la Afrika wa Kaskazini Mashariki ya Pacific.
Balozi Seif alisema suala la ajira hivi sasa limekuwa likizingatia zaidi muajiriwa katika Taasisi yoyote ile mbali ya ujuzi wake wa kitaalamu lakini pia unahusishwa na ufahamu wa suala la mtandao wa mawasiliano ya kompyuta.
Alieleza kwamba jamii inapozungumzia suala la sayansi na Teknolojia kwa sasa sio Physics na Chemistry lakini hata fani ya mitandao wa mawasiliano na Kompyuta imepewa nafasi kubwa zaidi ambayo pia inatoa fursa ya kurahisisha masomo hayo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwataka walimu na wanafunzi watakaobahatika kupatiwa Kompyuta na vifaa hivyo katika awamu ya kwanza kuhakikisha kwamba wanavitunza katika mazingira yatakayoviwezesha kudumu kwa muda mrefu zaidi.
Alisema hatua hiyo kwa kiasi kikubwa itaendelea kuwapa moyo watu, Mashirika na hata Taasisi zinazoamuwa kujitolea kusaidia vifaa na miradi mbali mbali katika sekta ya elimu.
Balozi Seif aliushauri Uongozi wa skuli mbali mbali nchini kufikiria kujenga vyumba maalum vitakavyokuwa na sifa ya kuwekwa kwa vifaa vya Kompyuta pale wakati utakaporuhusu kufanywa hivyo.
Mapema Naibu katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Nd. Abdulla Mzee Abdulla alisema awamu ya mwanzo ya msaada huo wa Kompyuta, Vifaa vyake pamoja na baadhi ya vitabu itaelekezwa kwa skuli 15 za Msingi ,Sekondari na baadhi ya vituo vya elimu Unguja na Pemba.
Nd. Mzee alizitaja skuli na vituo hivyo kuwa ni pamoja na Mtende, Chuo cha Sayansi ya Afya,Chuo cha Hoteli na Utalii, Kampuni ya Zitec itakayojishughulisha na matengenezo ya vifaa hivyo pamoja na Skuli ya Makunduchi.
Nyengine ni Kituo cha PSI, Skuli ya Alraudha, Utaani, Vitongoji, Kengeja, Vikokotoni, Kitope Lumumba, Mchanga Mdogo pamoja na skuli ya Sekondari ya Tumekuja.
Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Ali Juma Shamhuna ameishukuru Klabu ya Rotari ya Seattle Nchini Marekani pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa juhudi wanazochukuwa katika kuimarisha sekta ya elimu hapa Zanzibar.
Balozi Seif katika ziara yake ya mwezi Novemba mwaka jana Mjini Seattle Nchini Marekani alipata fursa ya kukitembelea kituo cha uungaji na matengenezo ya Kompyuta { Inter Connection } cha Rotary Clabu katika mji huo .
Mkurugenzi wa Kituo hicho Bwana Charles Brennik kupitia Klabu hiyo alitoa tamko na ahadi ya kuisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Kompyuta 2,500 kwa ajili ya maskuli mbali mbali hapa Zanzibar.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitembelea Mradi wa Ujenzi wa Skuli ya msingi, Vyoo pamoja na Tangi la Maji katika Kijiji cha Kiwengwa unaofadhiliwa na Mradi wa Kimataifa wa Give kutoka Nchini Marekani.
Wanafunzi 46 wa vyuo na skuli mbali mbali za Sekondari kutoka Nchini Marekani wamepiga kambi kwa zaidi ya wiki moja sasa katika Kijiji cha Kiwengwa wakiendelea na kazi mbali mbali za kujitolea katika ujenzi wa Skuli hiyo.
Kiongozi wa Wanafunzi hao Bwana Criss Backam alimueleza Balozi Seif kwamba wanafunzi hao ni mkupuo wa kwanza katika kuendeleza mradi huo katika awamu ya kwanza ya ujenzi huo iliyoanza mwezi Mei, Juni na kumalizia mwezi wa Septemba.
Bwana Criss alisema awamu ya pili ya wanafunzi hao itaingia mwezi Disemba na kuendelea na ujenzi huo hadi Mwezi Febuari mwakani ambapo alisema taaluma ya matumizi ya chupa za maji iliyobuniwa Nchini Nicaragua Amerika ya Kusini katika ujenzi huo inatumika ili kutunza mazingira ya kijiji hicho.
Akitoa shukrani zake Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Kitope aliwapongeza wanafunzi hao kutoka Marekani kwa uamuzi wao waliochukuwa wa kusaidia maendeleo ya Elimu katika Visiwa vya Zanzibar.
Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini juhudi hizo zenye nia ya kuwakomboa wananchi hasa watoto wa vijijini ambao kwa muda mrefu walikuwa wakikosa fursa muhimu za kielimu kutokana na mazingira yao ya kimaisha.
Wanafunzi hao wa Skuli mbali mbali za Sekondari Nchini Marekani wanatarajiwa kuondoka Zanzibar kwa kupitia Dar es salaam na Arusha ili kuona sehemu za kihistoria pamoja na mbuga za Taifa kabla ya kurejea nchini kwao siku ya Ijumaa.