Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Dkt Shein:Uimarishaji Miundombinu ya Usafiri wa Anga Nchini, Unalenga Kuhakikisha Huduma katika Sekta hiyo Zinakidhi Viwango.

$
0
0
STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                                                                16 Mei, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema upanuzi na uimarishaji wa miundombinu ya usafari wa anga unaofanyika hivi sasa umelenga kuhakikisha kuwa huduma za usafiri zinazotolewa Zanzibar zinakidhi viwango vya ubora wa huduma hizo kimataifa pamoja kuzingatia viwango vya usalama vinavyotakiwa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema hayo leo wakati akizungumza na ujumbe wa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO) ulioongozwa na Katibu Mkuu wake Bwana  Benjamin Raymond.  
Aliuambia ujumbe huo kuwa huduma za viwanja vya ndege na usafiri wa anga kwa ujumla, kama ilivyo kwa nchi nyingine ni muhimu kwa uchumi wa Zanzibar na ndio maana Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kwa nyakati tofauti kuimarisha sekta hiyo.
Alifafanua kuwa mwenendo wa usafiri wa anga nchini unaonesha kuongezeka kwa abiria mwaka hadi mwaka ndio maana Serikali imeamua kufanya upanuzi mkubwa wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar na kwamba imo mbioni kuanza upanuzi wa uwanja wa ndege wa Pemba ili nao uweze kutoa huduma wakati wote.
“hivi sasa tunapokea watalii wapatao 200,000 kwa mwaka lakini matarajio yetu ni kufikia watalii 500,000 ifikapo mwaka 2015 lakini hata hivyo baada ya upanuzi wa uwanja tunatarajia abiria kuongezeka kufikia kati ya milioni 1.5 na milioni 2”Dk. Shein alifafanua.
Kwa hiyo alieleza kuwa ziara ya ujumbe huo umekuja wakati muafaka kwa kuwa utapata fursa kuona jitihada za Serikali katika kuimairsha sekta ya usafiri wa anga Zanzibar na Tanzania kwa jumla na kuongeza ushirikiano kati ya ICAO na nchi yetu.

“Ziara yenu imekuja wakati huu muhimu tunapopanua miundombinu ya uwanja wetu wa ndege wa Zanzibar na tungependa kuona ICAO inasaidia kwa namna mbalimbali ili kuhakikisha usalama wa viwanja vyetu ikiwemo kuijengea uwezo Mamlaka ya Viwanja vya Ndege pamoja na kutupatia vifaa vya kutolea huduma katika viwanja hivyo kwa manufaa ya watumiaji wote wa usafiri wa anga ”Dk. Shein alisisitiza.
Dk. Shein aliuhakikishia ujumbe huo ambao ulijumuisha pia Mkurugenzi wa ICAO Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika Bwana Mashesha Belayneh kuwa Zanzibar imejidhatiti kuhakikisha kuwa usafiri wa anga unakuwa salama na wa raha wa watumiaji wake na ili kufikia lengo hilo ipo haja kwa ICAO kuzidisha ushirikiano na Zanzibar.
Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) Bwana Benjamin Raymond ameihakikishia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa shirika lake litaendelea kushirikiana nayo katika kuhakikisha kuwa hali ya usalama wa anga nchini unazidi kuimarika.
Amesema ujumbe wake umefika Zanzibar kuangalia jinsi shirika hilo linavyoweza kushirikiana na Zanzibar kukabiliana na changamoto zinaoendana na kupanuka kwa haraka kwa sekta ya usafiri wa anga ikiwemo suala la usalama wa usafiri huo.
Alieleza kuwa kuna kila dalili za usafiri wa anga kupanuka kwa haraka Zanzibar kutokana na kupanuka kwa sekta ya utalii pamoja na uwekezaji unaovutia watu kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni.
Kwa hiyo alieleza kuwa anaichukulia kwa uzito mkubwa rai aliyotoa Mheshimiwa Rais ya kutaka shirika hilo kufanyakazi kwa karibu na Serikali ya Zanzibar katika kusaidia kuimarisha usalama wa usafiri wa anga nchini.
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na viongozi wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano wakiongozwa na Waziri wake Mhe Rashid Seif Suleiman,viongozi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) na viongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar(ZAA).  

Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 
  E-mail: saidameir@ikuluzanzibar.go.tz

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>