Na Masanja Mabula,Pemba
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Mhe.Vuai Ali Vuai, amewataka wanaCCM kutowafumbia macho viongozi wanaokwenda kinyume na matakwa ya chama.
Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na baadhi ya viongozi wa sekretarieti za CCMo kuanzia ngazi ya tawi, wadi, jimbo na wilaya wa wilaya ya Micheweni.
Alisema lengo la CCM ni kudumisha amani, umoja na mshikamano ndani na nje ya chama na kutaka kutowapa nafasi viongozi wanaojihusisha na majungu kama wanataka kuimarisha chama.
"Wekeni vikao vya mara kwa mara kujadili changamoto ndani ya chama kwa kushirikianaa viongozi wa serikali kwani nao wanafanya kazi kutekeleza ilani ya CCM,” alisema.
Aidha alisema ushirikiano huo utasaidia kutengeneza njia itakayotumika kuleta ushindi katika uchaguzi mkuu wa 2015.
Alisema uimara wa CCM unategemea uimara na uhai wa wanachama na jumuiya zake na kuwaomba viongozi hao kuwahimiza wanachama wa chama hicho kulipia ada ili kukifanya chama kuendesha shughuli zake kwa ufanisi.
"Tusingoje wakati wa uchanguzi ili kulipia ada zetu lengo ni kutaka kupata kura, hivyo tunatakiwa kujiwekea mipango ya kuhakikisha kwamba kila mwananchama pamoja na jumuiya zake analipia kadi kwa wakati,” alisema.
Aliwataka wanaCCM kukitendea haki chama chao kwa kuhakikisha wanashiriki katika mchakato wa kupiga kura kupitisha rasmu ya katiba wakati utakapofika.
Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa kaskazini Pemba, Mberwa Hamad Mberwa, alisema CCM mkoa huo wako pamoja na viongozi wa juu wa chama na kwamba wanajianda kwa ajili kupiga kura ya maoni kuhusu katiba mpya.