Na Fatina Mathias, Dodoma
WAZIRI Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda, amesema serikali kwa kushirikiana vyombo vya usalama vya nje, itahakikisha inawabaini watu wanaowashambulia viongozi wa dini na watalii mjini Zanzibar .
Kauli hiyo aliitoa jana alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum, Betty Machangu (CCM) katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu.
Mbunge huyo alitaka kujia hatua ambazo serikali imechukua dhidi ya matukio ya mauaji hayo mjini Unguja.
“Hivi karibuni tulishuhudia mauaji ya Padri kule Zanzibar, lakini pia tumeshuhudia pia wawekezaji Wafaransa wakiuawa na maiti zao kutumbukizwa kwenye kisima,lakini tumeshuhudia Masheikh na walimu wa kujitolea wakimwagiwa tindikali, Waziri Mkuu matukio yote hayo serikali imechukua hatua gani,”alihoji.
Pinda alisema serikali imejipanga vizuri kwa kujaribu kushirikiana na vyombo vya nje ili kuendelea kuwabaini wahusika wa matukio hayo ikiwa ni pamoja na vyanzo na sababu ili kuyakabili kabla hayajatokea.
“Na kwa taarifa nilizonazo hata baadhi ya matukio ambayo yalikuwa yafanyike tumeweza kuyakabili kabla ya kutokea,hivyo niwahakikishie Watanzania na hata watalii kwa ujumla kwamba hali kwa kweli ni shwari kwa ujumla wake na serikali tumeshachukua hatua stahiki na tutaendelea kuwa macho zaidi kukabiliana na hali hii ambayo inajitokeza hapa na pale,”alisema.
Katika swali lake la msingi Machangu alihoji vikundi vya uharifu na kigaidi vilivyoibuka mkoani Mtwara,Tanga,Iringa na Dar es salaam .
Alitolea mfano wa vikundi vya Dar es Salaam vya Kontau, Jenerali Nyau, Komando Yusuph, Sure, Panya Road, Mbwa Mwitu, Kiboko Msheli na waasi M23 ambavyo ni vikundi vya vijana wadogo wanaovamia wananchi mchana na kuwaibia.
Alisema kwa upande wa vikundi vya Tanga na Mtwara ni vikundi vya kigaidi ambavyo vilifichwa msituni kupewa mafunzo ya kigaidi ambapo inasemekana wako vijana wanaopelekwa Somalia kwa mafunzo zaidi ya kigaidi.
Pinda alikiri kuibuka kwa vikundi hivyo na kusema mara nyingi tatizo hilo linapotokea serikali huchukua hatua za haraka kujaribu kudhibiti tatizo hilo .
Aliwataka vijana kujiepusha kujiingiza katika vitendo ambavyo baadaye vinaweza vikawaingiza katika mgongano na vyombo vya dola.
Kuhusu vikundi cha Mtwara, Pinda alisema jambo hilo linawezekana japo hakuwa na taarifa hizo hivyo akamuomba Machangu kumpa muda ili aweze kuzungumza na wahusika wa Mtwara ili kuweza kupata uhalisia wa tukio hilo .
Wakati huo huo,Mbunge wa Musoma mjini, Vicent Nyerere, alimtaka Mhe. Pinda kutoa kauli ya serikali katika kusuluhisha mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa Makoko Musoma mjini na kikosi cha jeshi la Wananchi cha 27KJ.
Nyerere alisema maeneo ya kambi za jeshi hayakuwa yamewekwa mipaka iliyokuwa ikitambulika vizuri na wananchi na kwa sababu hayakuendelezwa kwa muda mrefu wananchi waliamua kuingia katika maeneo hayo huku halmashauri kwa kujua ama kutokujua wakiwaacha wakiendelea na shughuli zao.
Akijibu swali hilo, Mhe. Pinda alisema vyombo vya ulinzi hasa Jenshi la Wananchi mara nyingi hupangwa katika maeneo husika kutokana na sababu fulani za kiulinzi hivyo kama eneo limechwa kwa muda mrefu na kuonekana halina matumizi lazima watu wataingia katika eneo hilo na kufanya shughuli zao.
“Kinachonisumbua mimi ni kwamba inakuwaje jeshi ambalo mnatambua eneo lenu mngoje mpaka kaya 300 zijenge bado hamjashituka,zimekamilika ndipo mnasema eneo letu mimi kidogo hilo linanisumbua,” alisema