Na Khamis Mohammed
UELEWA mdogo wa wanajamii pamoja na imani potofu walionayo baadhi ya watu kuhusu dhana nzima ya uzazi wa mpango, imeelezwa kuwa ni changamoto kubwa inayopelekea wanawake wengi kutojitokeza kutumia uzazi wa mapango.
Hayo yameelezwa na Dk.Sebastian Macrice, wakati wa mdahalo juu ya uzazi wa mpango kwa maendeleo, uliofanyika ofisi za Kitengo Shirikishi cha Afya ya Uzazi na Mtoto, Kidongochekundu mjini hapa.
Dk.Macrice, alisema, baadhi ya wanawake wamekuwa wakitaka kushiriki uzazi wa mpango, lakini, kutokana na kuwahofia waume zao, wamejikuta wakipata huduma hiyo kwa kujificha kinyume na malengo yanayokusudiwa.
Alisema, wanaume wengi si washiriki wazuri katika suala la afya ya uzazi, hatua inayosababisha wanawake wanaoamini uzazi wa mpango kuamua kutumia njia za usiri na hivyo kukosekana maridhiano baina ya pande hizo.
Alisema, suala hilo limefanya baadhi ya ndoa kuvunjika au kukumbwa na migogoro isiyotarajiwa ikiwemo tuhuma za kutembea nje ya ndoa.
Dk.Macrice, alisema, hivi sasa ni asilimia 27% ndiyo inayotumia uzazi wa mpango na kwamba lengo linalokusudiwa ni kufikia angalau asilimia 60 ifikapo mwaka 2020.
"Safari bado ni ndefu, vifo vinavyotokana na uzazi ni vingi, lazima jamii ibadilike," alisema.
Alisema, lengo hilo linaweza kufikiwa kwa kushirikiana na wanajamii katika kupata elimu sahihi juu ya uzazi wa mpango sambamba na kuepuka uzazi wa papo kwa papo.
"Uzazi wa papo kwa papo unapelekea kuregea kwa fuko la uzazi au wakati mwengine kupelekea kutoka damu nyingi kwa mama mjamzito, ni hatari", alieleza.
Aidha, alieleza, hata ulemavu wanaopata wamama ambao hawajajiandaa kubeba ujauzito nao unaweza kuepukika kwa kutumia uzazi wa mpangilio na hivyo kupunguza vifo vya mama na watoto.
Dk.Macrice, alisema, uzazi wa mpangilio unatoa uhueni kwa familia katika kuwatunza watoto hao pamoja na kuwapatia huduma nzuri, kwa vile panakuwepo na maandalizi ya kiuchumi kabla ya kupokelewa mtoto mpya.
Naye Sheikh Ismail Asaakher kutoka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar, alisema, uislamu haukatazi uzazi wa mpango, lakini, inachosisitiza ni njia ambazo hazitaleta athari baina ya wazazi.
"Bwana Mtume ametuhimiza tuoane ili tuwe wengi, lakini, kwa kuwatimizia watoto mahitaji yao ya lazima," alisema.
Hivyo, alisema, ni juu ya wazazi kuridhiana bila ya kupoteza haki ya mwengine na kwamba mtoto ni zawadi ambayo inatakiwa kupatiwa huduma.
Mapema, Mwakilishi kutoka UMATI, Mwanajuma Salum Othman, alisema, moja ya tatizo kwa nchi zinazoendelea ni kuongezeka kwa idadi ya watu, hivyo uzazi wa mpango unatoa nafasi kudhiti hali hiyo.
Hata hivyo, alisema, jamii bado haijaelewa umuhimu wa uzazi wa mpango kulingana na rasilimali ndogo wanayowajibika nayo katika maisha ya kila siku.