Na Mwandishin Wetu.
WANANCHI mbali mbali wameeleza kusikitishwa kwao juu ya suala la upandaji wa bei za bidhaa zikiwemo nguo,kwa ajili ya matayarisho ya sikukuu.
Walisema bei za bidhaa aina hiyo katika kipindi hichi cha mwezi mtukufu wa ramadhani zimekuwa zikiongezeka siku hadi siku bila ya kufahamu sababu kuu za kuongezeka kwa bei hizo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mmoja wa wanunuzi wa bidhaa hizo Mwanaisha Mgeni Hassan alisema wafanya biashara wengi wameonekana kuuza nguo,viatu na bidhaa nyengine zinazohitajika katika kipindi cha sikukuu ambapo jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na serikali kuhusu suala hilo.
Alisema hali hiyo inapelekea kutokuwa na imani na serikali pamoja na wafanyabiashara kwa sababu kuna baadhi ya wananchi hawana uwezo wa kununua kiwango hicho ambacho kimezidishwa.
Alisema kuna baadhi wanakuwa na familia kubwa ya kuwahudumia lakini wanashindwa kwa kuwa kila nguo moja inauzwa shilingi 35,000 na shilingi 50,000.
Nae mfanyabiashara wa nguo za watoto wa Darajani Hassan Mussa Hassan alisema ni kweli kwamba bei za nguo zipo juu na baadhi ya wateja wengine wanashindwa kununua kwa kutoweza kumudu gharama hizo.
Aidha alisema sio kweli kama inavyodaiwa kuwa wafanyabiashara wanazidisha bei za nguo kila ifikapo katika kipindi cha mwezi mtukufu wa ramadhani na kusema kuwa bei inayouzwa mwanzo ndio inayouzwa katika kipindi hicho.
Hata hivyo alisema sababu inayowafanya kuuza bei ya juu ni kutokana ununuzi wa dola inakuwa kubwa na wakifika nje inakuwa imeshuka ndipo wanapoangalia ile thamani halisi ya bei waliyonunulia.
Pia alisema sababu nyengine ni mamlaka ya TRA upande wa Dar-es-Saalam kuwatoza ushuru kwa mizigo inapofika hapo na inapotolewa kuja Zanzibar pia inalipiwa.