Na Kauthar Abdalla
VIONGOZI na watendaji wa serikali wametakiwa kuongeza nguvu katika kuunga mkono kwa vitendo kampeni ya safisha Zanzibar ili kuhakikisha inafikia lengo.
Wakizungumza katika kampeni hiyo wakaazi wa kijiji cha Nungwi, walisema kufanya hivyo kutaongeza ari ya utendaji kwa washirika wa maendeleo ambao wameanzisha mpango huo ili kukuza utalii wa kimazingira.
Mmoja ya wanakijiji hao, Kazija Silima, alisema endapo hali ya mazingira itakuwa ya kuridhisha idadi ya watalii wanaotembela kijiji hicho itaongezeka.
Alisema mpango huo unaoendeshwa na jumuiya ya ZANREC umeanzishwa baada ya Zanzibar kutangazwa kuwa katika kiwango kisichoridhisha cha usafi ambapo imesababisha kupokea watalii wa daraja la chini hali inayotishia kuathiri uchumi wa Zanzibar kwa kuwa sekta ya utalii ndio inayotegemewa.
Alisema kijiji cha Nungwi kimekuwa kikipokea wageni wengi lakini wanakijiji wanapata hofu ya kupungua kiwango wageni hao kutokana mazingira yake kutokuwa safi .
Nae Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini wa Jumuiya la Labayka Development Fund, Haji Khamis Haji, alisema katika kudumisha dhana ya mtu na mazingira ni vyema kuzingatia madhara ya uchafu ambayo athari yake ni kubwa.