Na Laylat Khalfan
ZAIDI ya shilingi milioni 300 zimetumika kwa ajili ya mradi wa kuangamiza kunguru weusi kuanzia 2012-2013.
Hayo yalielezwa na Msaidizi Mratibu wa huo, Salim Ali Khamis, alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Maruhubi.
Alisema mradi huo unatekelezwa kwa fedha za wafadhili kutoka serikali ya Finland .
Alisema lengo la mradi huo ni kupunguza idadi ya kunguru weusi ambao wanasababisha kero na adha kwa wananchi na maisha ya ndege wengine muhimu.
Alisema kwa kiasi kikubwa mradi huo umefanikiwa ambapo kiasi cha kunguru 168,000 wameangamizwa kwa Unguja na Pemba 32,000.
Hata hivyo, alisema mradi huo unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kuibiwa kunguru hao wanapoingia katika mtego.
Aidha alisema kuna baadhi ya watalii huwa wanawanasua kunguru waliongia kwenye mitego kwa madai kwamba wanateswa.
Baadhi ya wananchi wa maeneo ya mjini waliupongeza mradi huo wakisema umesaidia kupunguza idadi ya kunguru ambao walikuwa kero kwa mifugo yao ikiwemo kuku.