Na Haji Nassor, Pemba
Mfanyabiashara wa kuku katika soko kuu mjini Chake Chake Pemba, Amour Mohamed Salim (40) (Cheupe), amevamiwa na majambazi kumpiga kwa vitu vizito usiku wa kuamjia jana.
Alisema majambazi hayo yalikuwa yamevalia sare zinazofanana na za JKU.
Tukio hilo lilitokea nyumbani kwake Chambani wilaya ya Mkoani Pemba, baina ya saa 7:00 na saa 8:00 usiku, wakati akiwa amelala na familia yake.
Mashuhuda wa tukio hilo, walisema awali walisikia kishindo kikubwa na mlio kama wa risasi, na kufuatiwa na sauti za watu waliomtaka Cheupe atoe fedha.
Hata hivyo, walisema wakati wakijitayarisha kutoka kwenda kumsaidia, waligundua kuwa nyumba zao zimefungwa kwa nje na kushindwa kutoka nje hadi alipotokea jirani mwenzao kuwafungulia na walipofika kwa mfanyabiashara huyo majambazi hayo yalikwishatokomea.
“Sisi tulisikia toa pesa, nakuua, toa pesa, kisha tukasikia jamani nauliwa, nauliwa lakini tulipotaka kwenda kutoa msaada, tuligundua nyumba zetu zimefungwa kwa nje,” alisema Mohamed Said Msiu mmoja wa mashuhuda hao.
Alisema majambazo hayo yalipora nguo zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye mabegi matatu,simu ya mkononi, ufunguo wa skuta, fedha taslimu shilingi 120,000 na vitu nyengine vya thamani.
Mke wa mfanyabiashara huyo,Mariyam Salim Suleiman, alisema baada ya mume wake kuvamiwa na watu, walimtaka awape shilingi milioni 10 vyenginevyo wengemua.
“Tupatie shilingi 10 milioni, ili tukuachie uhai wako, au sisi tunakua,” alisema Mariyam akiwanukuu majambazai hayo.
Nae mfanyabiashara huyo, alisema watu hao walivunja mlango kwa kutumia mawe na vifaa vya ujenzi.
“Mimi najisikia nafuu sana na kwa kweli hawakuniathiri sana, lakini nguo za mke wangu na fedha taslimu wameondoka nazo,” alisema.
Cheupe alifikishwa hospitali ya Chambani na kupatiwa huduma ya kwanza, ambapo baadae alikwenda kituo cha polisi Mtambile na kupatiwa fomu ya matibabu (PF3) na kwenda hospitali ya Chake Chake kutibiwa.