Na Joseph Ngilisho,Arusha
MUUZA nyama ,Lucas Lomayany Molel (37) mkazi wa Ilboru,jijini hapa,anatafutwa na polisi kwa kosa la kumuua mkewe wa ndoa,Agness Lucas (24) kwa kumkata mapanga, kwa kile kinachoelezwa kuwa ni wivu wa mapenzi.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jana nyumbani kwa mtuhumiwa,ambapo huyo baada ya kutekeleza mauaji hayo aliufunika mwili wa marehemu mkewe na kisha kuendelea kulala nao kitandani hadi alfajiri alipofanikiwa kutoroka.
Mdogo wa mtuhumiwa,William Lomayany, alisema kabla ya mauaji hayo, kaka yake alikuwa na tabia ya kumpiga mkewe na aliwahi kumjeruhi mara kadhaa kwa kumkatakata kwa sime.
Akisimulia mauaji hayo,Williamu alisema usiku wa kuamkia jana majira ya saa 4:00,mdogo wake alirejea nyumbani kwake na kukuta mkewe hayupo.
Alisema aliamua kumsubiri bila kulala hadi majira ya saa 6:00 usiku ndipo mkewe aliporejea.
Alisema marehemu baada ya kufunguliwa na kuingia ndani ,alivua nguo zote na kubakiza nguo ya ndani ambapo alijifunga kanga na kutaka kulala,hata hivyo mtuhumiwa alimfuata chumbani na kuanza kumhoji kujua anakotokea.
Alisema wawili hao walianza kugombana kwa maneno ,lakini baada ya muda hali ya utulivu ilirejea ndani ya chumba hicho, lakini majira ya saa moja asubuhi jana walipata taarifa za mauaji hayo.
Alisema mtoto wa kwanza wa mtuhumiwa, alitwaye Jesca Lucas (11) ndiye aliyekuwa wa kwanza kufungua mlango na kutoa taarifa kwa majirani kuwa mama yake amelala huku damu zikiwa zimetapakaa juu ya godoro.
Alisema baada ya taarifa hiyo ndugu wa karibu wakiwemo majirani waliingia ndani ya chumba hicho na kukuta mwili wa marehemu ukiwa umelala chini ya dimbwi la damu ukiwa utupu.
Akizungumza mbele ya askari polisi waliofika kushuhudia mwili wa marehemu, mtoto wa mtuhumiwa,alisema baba yake alimwamsha usiku na kumwambia aje kufunga mlango baada ya kutoka ndani akijua huendea alikuwa anaenda kazini.
“Baba aliniamsha usiku karibia kunakucha akaniambia nifunge mlango aliondoka bila kusema chochote ila jana usiku baba alikuwa akimpiga mama na alinipiga na mimi wakati namwambia amsamehe,aliniambia nilale,” alisema.
Mauaji hayo yamesababisha mzozo mkubwa kutoka kwa ndugu wa marehemu ambao walivamia msiba na kuwataka ndugu wa mtuhumiwa wawapatie mwili wa marehemu ndugu yao wakauzike ,hata hivyo upande wa pili ulizuia.
Kamanda wa polisi mkoani hapa,Liberatus Sabas, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa bado uchunguzi unaendelea.