Na Kadama Malunde,Shinyanga
Waziri Mkuu,Mizengo Pinda, amewataka viongozi wa dini kuendelea kushirikiana na serikali na kuliombea taifa kutokana na kuanza kuibuka matukio ya ugaidi ambayo yanatishia amani iliyopo.
Akizungumza kwa niaba ya Pinda, Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,Mahusiano na Uratibu, Stephen Wasira, alisema viongozi wa dini hawanabudi kuunganisha nguvu kwa pamoja kulaani vikali vitendo hivyo viovu ,kwani ni hatari kwa taifa.
Alikuwa akizungumza katika harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa la parokia ya Usanda ya Papa John Paul wa II lililopo Tinde mkoani Shinyanga.
Aidha alipongeza jitihada kubwa zinazofanywa na taasisi za dini kuwekeza kwenye elimu,afya na huduma nyingine muhimu katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Awali katika ibada iliyoongozwa na Makamu wa Askofu jimbo Katoliki la Shinyanga,Padri Sospeter Sholle,alisema kuporomoka kwa maadili katika jamii ni mambo yanayochangia kupata viongozi wasiowaadilifu, wabinafsi na waroho wa madaraka.
Akiwasilisha ujumbe uliotolewa na baraza la maaskofu Tanzania kuhusu katiba mpya, Padri Shole, alisema bunge maalumu la katiba linatakiwa kuzingatia maoni ya rasmu ya pili ya katiba,kwani Watanzania wanahitaji kuwa na katiba itakayojali utu wa kila mmoja,kuzuia matumizi mabaya ya madaraka na ufisadi.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa kanisa hilo ambalo litaitwa Papa John Paul wa II, Padri Dk. Emmanuel Makolo, alisema ujenzi wake mpaka kukamilika unatarajia kugharimu zaidi ya shilingi milioni 244 na kuwaomba Watanzania na wadau mbalimbali kuchangia ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Mgeni rasmi katika harambe hiyo angia shilingi milioni 6.