Na Mwandishi wetu
Makachero wa Jeshi la Polisi Zanzibar, wamefanikiwa kumtia mbaroni mmoja wa washukiwa wa matukio ya tindikali visiwani hapa, alietajwa kwa jina la Alawi Mohammed Silima (25) mkazi wa Fuoni Melinne nje kidogo ya mji wa Zanzibar .
Ofisa Habari Mkuu wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Inspekta Mohammed Mhina, alisema mtuhumiwa anahusishwa na tukio la kummwagia tindikali Sheha wa shehia ya Tomondo mjini Zanzibar,Mohammed Omar Saidi Kidevu kabla ya kutoweka.
Alisema mtuhumiwa huyo ambaye kwa muda mrefu alikuwa akisakwa na polisi kwa kuhusika na tukio hilo, alikamatwa juzi usiku akiwa mafichoni katika eneo la Fuoni baada ya taarifa za kiintelijensia kubaini kuwepo kwake.
Alisema bado makachero hao wanaendelea kumhoji mtuhumiwa huyo kwa lengo la kuubaini mtandao mzima wa matukio mbali mbali yakiwemo ya tindikali yaliyotokea siku za nyuma visiwani hapa.
Kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kunatokana na taarifa za siri za raia wema ambapo jeshi la polisi lilikua likiendelea na upelelezi wa chini kwa chini wa kumbaini mtuhumiwa na mahali alipojificha.
Baadhi ya wananchi wa Zanzibar wamepongeza kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na kuliomba jeshi la polisi kuendelea na juhudi zake za kuwasaka watuhumiwa wengine wanaohusika katika matukio menginne kama hayo siku za nyuma.
Tukio la kumwagiwa tindikali kwa sheha huyo, lilitokea majira ya saa 2.45 usiku wa Mei 22 mwaka jana, wakati sheha huyo alipokuwa akirudi nyumbani akitoka kuchota maji nyumba ya jirani. na kujeruhiwa vibaya mgongoni, kifuani, sikio na jicho la upande wa kulia.