Na Mwandishi wetu
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, amesema rasimu ya sera ya diaspora iko kwenye hatua za mwisho na muda si mrefu itaingizwa kwenye utaratibu wa kiserikali ili hatimaye iweze kuwasilishwa kwenye Baraza la Mawaziri.
Akizungumza na Watanzania wanaoishi Uingereza kwenye mkutano uliofanyika ubalozi wa Tanzania jijini London, mwishoni mwa wiki, Pinda, alisema mchakato wa kuandaa rasimu hiyo ulihusisha wadau wengi kwa kadri ilivyowezekana ili kupata wigo mpana wa suala zima la diaspora.
“Katika hatua za awali, mbali ya ofisi yangu na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, tuliwashirikisha kwa karibu Umoja wa Wanadiaspora waliorudi Tanzania (Tanzania Diaspora Initiative) na wanadiaspora kutoka Uingereza, Marekani, China, Oman, India na Afrika Kusini ili kupata uzoefu wao kutokea huko waliko,” alisema.
“Baadaye tukawapelekea wataalamu ambao ni Profesa Samuel Wangwe wa REPOA, Profesa Joseph Semboja wa Uongozi Institute na Profesa Faustine Kamuzora wa Chuo Kikuu cha Mzumbe kila mmoja kwa wakati wake na kuwaambia waichanechane kadri wawezavyo na kisha watupe mrejesho wao,” alisema.
Aliwataja wadau wengine muhimu waliohusishwa kwenye kuichambua rasimu hiyo kuwa ni Shirika la Kimataifa linaloshughulika na Wahamiaji (IOM) ambao wamebobea katika masuala ya wahamiaji katika nchi mbalimbali duniani.
“Kwa mtazamo wangu hii rasimu imekaa vizuri kwa sababu tumejitahidi kugusa kila eneo ambalo kwenu lilikuwa na umuhimu wa kipekee. Sasa hivi imeshawekwa vizuri kimfumo na inasubiri iingie katika utaratibu wa kiserikali,” alisema.
Wakati huo huo Pinda alisema serikali inaandaa kongamano la siku mbili litakalojadili mustakabali wa wana diaspora wa Tanzania kutoka nchi zote duniani ikiwa ni pamoja na kuwakutanisha na makampuni na wafanyabishara mbali mbali.
Alisema kongamano hilo ambalo limepangwa kufanyika Agosti 14-15, mwaka huu, linalenga kuitambulisha rasmi diaspora ama jamii ya Watanzania inayoishi ughaibuni kama wadau muhimu katika kuleta maendeleo nchini Tanzania . "Lengo letu hasa ni kutaka jamii ya Watanzania ielewe kwamba tunao Watanzania walioko nje ya nchi kwa maelfu na kuna sehemu mnaweza kuchangia katika maendeleo ya nchi," alisema.
Alisema katika kuitambua rasmi jamii ya wanadiaspora, serikali itapenda kujua wapo wangapi na wanafanya nini ambacho kama Sserikali itahitaji ujuzi auutaalamu wao, inaweza kuwapata.
Alisema kongamano hilo limeandaliwa kwa ushirikiano baina ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa pamoja na Umoja wa Wanadiaspora waliorudi nchini waitwao (TDI).
Akifafanua zaidi kuhusu taswira nzima ya Diaspora, alisema: "Sensa ya mwaka 2012 inaonesha katika kaya zote zilizohesabiwa Tanzania Bara kuna mtu mmoja au zaidi ambaye yuko nje ya nchi. Hii ni sawa na asilimia 1.2. Kwa upande wa Zanzibar, hali iko tofauti sana . Wao ni mara mbili zaidi yaani kila kaya moja ina watu wawili na zaidi ambao wako nje ya nchi."
Alisema katika matokeo ya sensa, ilibainika kwamba wanadiaspora wanaotoka kwenye kaya za mikoa ya Tanzania Bara wako 116,670 wakati wanaotoka Zanzibar wanafikia 304,786.
“Idadi ya Watanzania walioko Diaspora ni 421,456 ni karibu sawa na nusu milioni. Idadi hii si ndogo, ni kubwa. Na kama kundi hili lingetumika vizuri, fedha waliyonayo ambayo wanaituma kutoka nje, ingesaidia kuendeleza taifa letu,” alisema.
Alitumia fursa hiyo kuwaelezea kuhusu mchakato wa katiba ulivyoenda na ulipofikia, maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na uchaguzi mkuu.
“Kama serikali tunajiandaa kwa lolote litakaloamuliwa na Bunge Maalum la Katiba. Kikubwa tunachoomba ni kuwa na mchakato wa amani hadi uchaguzi mkuu ufike,” aliongeza.
Aliwataka wanadiaspora waendelee kuiombea nchi ili ipate wagombea wenye kujali maendeleo ya watu kuliko kitu kingine chochote.
Endeleeni kuiombea nchi yetu ili tupate watu waadilifu, watu ambao wanajali watu wa hali ya chini na wenye kutaka maendeleo ya nchi kwanza kuliko vitu vingine.
“Endeleeni kuiombea nchi yetu amani, tuendelee kumuombea Rais Kikwete ili amalize kipindi chake vizuri na akabidhi kijiti kwa mwingine salama,” alisema.