Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

‘Watoto 11,216 wanaishi bila ya uangalizi wa wazazi’

$
0
0
Na Hassan Hamad,OMKR
WATOTO milioni 153 wanaishi bila ya uangalizi wa wazazi duniani kote, huku Tanzania ikiwa na watoto wa aina hiyo wapatao 11,216.

Hayo yameelezwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, wakati akifungua mkutano wa kimataifa wa siku tano kwa nchi wanachama wa vijiji vya SOS, unaofanyika hoteli ya ZanzibarBeach Resort.

Pamoja na mambo mengine mkutano huo unajadili namna ya kukuza uelewa katika uendelezaji wa vijiji vya watoto vya SOS, pamoja na kutathmini mafanikio na changamoto zinazovikabili vijiji hivyo.

Alisema idadi ya watoto wanaokosa uangalizi wa wazazi imekuwa ikiongezeka kutokana na sababu mbali mbali zikiwemo kufariki kwa wazazi, hali ya umaskini, unyanyasaji na talaka.

Alisema matokeo ya hali hiyo ni kuongezeka kwa ajira za watoto ambapo  Zanzibar pekee inakisiwa kuwa na asilimia 9.2 ya watoto kati ya umri wa miaka mitano hadi 17 wanaojihusisha na ajira hizo.


Alisema katika kukabiliana na tatizo hilo, juhudi za pamoja zinahitajika kati ya taasisi za umma na binafsi, kuhakikisha haki za watoto zinalindwa, sambamba na kuzisaidia familia zenye watoto yatima na zinazoishi katika mazingira magumu.

Alisema serikali kwa upande wake inaridhishwa na kazi kubwa inayofanywa na SOS Zanzibar na Tanzania, na kuzitaka taasisi hizo kuzidisha bidii katika kuleta ufanisi.

Alielezea matumaini yake kuwa kampeni ya CARE FOR ME  iliyozinduliwa na vijiji vya SOS mwaka 2012, italeta faraja na mafanikio kwa kuwapatia watoto huduma bora zikiwemo za elimu.

Aliyashukuru mashirika ya misaada ya Norway (NORAD), Austria (ADA) na Denmark kwa kuunga mkono miradi ya SOS, hatua ambayo alisema inaisaidia serikali kukabiliana na matatizo yanayowakabili watoto.

Mapema akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa bodi ya vijiji vya SOS Zanzibar, Mohammed Bhaloo, alisema SOS Zanzibar inawahudumia watoto 800 kwa kuwapatia elimu bora, kupitia  skuli ya msingi na sekondari ya Hermann Gmeiner iliyo chini ya kijiji hicho.

Alisema SOS Zanzibar pia ina kituo cha afya ambacho hutoa huduma kwa watoto wa kijiji hicho pamoja na wananchi wa maeneo ya karibu ambapo zaidi ya wagonjwa 1,400 hupatiwa matibabu katika kituo hicho kwa mwaka.

Aliongeza kuwa pamoja na mambo mengine SOS Zanzibar kupitia mpango wake wa kuwajengea uwezo watoto, inazisaidia familia 180 zenye watoto 1000 Unguja na Pemba, ili ziweze kuimarisha huduma kwa watoto hao.

Akizungumzia kuhusu historia ya vijiji vya SOS Zanzibar, Bhaloo alisema azma ya kuanzishwa kwa vijiji hivyo iliasisiwa mwaka 1984 na kuanza kuwahudumia watoto kuanzia mwaka 1991.

Aliishukuru serikali na taasisi binafsi kwa ushirikiano wao katika kuunga mkono juhudi za vijiji vya SOS, na kwamba mafanikio makubwa yamepatikana tokea kuanzishwa kwa vijiji hivyo.


Mkutano huo wa siku tano unazishirikisha nchi mbali mbali zenye vijiji vya SOS zikiwemo Austria, Cameroon, Ethiopia, Malawi, Msumbiji,Morocco, Uganda, Afrika Kusini, Zambia, Zimbabwe, Tanzania na wenyeji Zanzibar.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>