Na Joseph Ngilisho,Arusha
SIKU chache baada ya Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Shabaan bin Simba, kutangaza uongozi mpya wa msikiti wa Ijumaa na msikiti wa Quba iliyopo jijinihapa,Sheikh wa msikiti wa Qiblatan,Sood Ally Sood (37), amejeruhiwa baada ya kushambuliwa kwa bomu la kurushwa kwa mkono nyumbani kwake wakati akila daku na kujeruhiwa vibaya.
Aidha mbali na Sheikh huyo,mtu mwingine aliyekuwa nyumbani kwake, aliyetajwa kwa jina la Muhaji Kifea (38) mkazi wa Sinza jijini Dar es Salaam, naye amejeruhiwa vibaya na wote wamelazwa hospitali ya mkoa Mount Meru kwa matibabu.
Sheikh huyo alijeruhiwa miguu yote miwili na mapajani huku Kifea akipata majeraha makubwa miguuni na kupoteza baadhi ya vidole vya miguu yote miwili.
Akizungumza hospitalini hapo, Sheikh Sood, alisema tukio hilo lilitokea nyumbani kwake eneo la majengo ya chini,usiku wa kuamkia jana majira ya saa 5:00 wakati yeye pamoja na mgeni wake wakila chakula sebuleni .
Alisema alishangaa kusikia mripuko mkubwa ulioambatana na vyuma na kujikuta akiwa na majeraha makubwa.
“Hawa watu kimsingi wanafahamika maana walishawahi kunitishia kupitia waraka wa maandishi pamoja na kunifyatulia risasi,” alisema.
Alisema siku tatu kabla ta tukio hilo alikoswa kuuawa kwa risasi na watu wasiofahamika wakati akitoka msikitini na kutoa taarifa kituo kikuu cha polisi jijiji hapa.
Akizungumzaia tukio hilo Mkuu wa Mkoa wa Arusha ,Magesa Mulongo,alichukizwa na kitendo hicho na kusema hatua zitachukuliwa kwa wahusika.
Aidha alisema polisi linawashikiwa baadhi ya watuhumiwa wa matukio ya mabomu.
Naye kamanda wa polisi mkoani Arusha, Liberatusi Sabasi ,alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa majeruhi bado wanaendelea na matibabu.
Mbunge wa Arusha mjini,Godbless Lema,alilitaka jeshi la polisi kurejesha amani jijini hapa kwa kulichukulia kwa umakini suala hilo.