Na Kija Elias, Moshi
MBUNGE wa jimbo la Vunjo, Augustino Mrema, amewataka viongozi wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA),kuacha kueneza propaganda chafu dhidi yake kwa kujipitisha jimboni mwake na kuwalaghai wapiga kura kwamba yeye ameahidi kuwaachia jimbo hilo.
Kauli hiyo ameitoa jana wakati akizungumza na vyombo vya habari katika mji mdogo wa Himo, wilayani Moshi mkoani humo.
Alisema malengo ya Ukawa sio katiba mpya kama ambavyo wengi walitarajia isipokuwa ni uchaguzi wa mwaka 2015.
Alisema tangu Ukawa watoke bungeni , wamekuwa wakienda kwa wananchi na ajenda yao ya katiba wameiacha badala yake wanazungumzia uchaguzi mkuu ujao.
Alisema baadhi yao wamediriki hata kuwaambia wananchi wa jimbo la Vunjo kuwa Mrema hatagombea tena ubunge jambo ambalo amelikanusha vikali.
Alisema bungeni ndio mahali sahihi pa kujadiliana namna ya kupata katiba mpya na sio kutoka na kwenda barabarani kama ambavyo Ukawa wamekuwa wakifanya.
Alisisitiza kuwa kinachotakiwa ni wajumbe wote kushiriki katika bunge maalum la katiba na sio kukimbia kazi hiyo kwa sababu waliaminiwa na Watanzania.