STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 13 Agosti, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema Karakana ya Serikali ya Matrekta ndio uti wa mgongo wa utekelezaji wa Mpango wa Serikali wa Kuimarisha Kilimo hususan kilimo cha mpunga cha umwagiliaji.
Akizungumza na watumishi wa Karakana hiyo iliyopo Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar leo Dk. Shein aliwaeleza watumishi hao kuwa Serikali inaitegemea sana karakana hiyo kwa kuwa ndio inayoshughulikia matengenezo ya vifaa vya kilimo yakiwemo matrekta.
Kwa hiyo alibainisha kuwa mpango wa Serikali ni kuiimarisha karakana hiyo kwa kuipatia vifaa vipya na mahitaji mengine kwa sasa na kwa siku zijazo inataka karakana hiyo kuwa kiwanda cha kuunganisha matrekta kwa matumizi ya humu nchini na nje.
“lengo letu ni kuimarisha karakana hii... matrekta 50 yaliyopo sasa pamoja na mashine za kuvunia mpunga zinategemea karakana hii kwa matengenezo ”alifafanua Dk. Shein.
Aliongeza kuwa wakulima wa mpunga wamehamasika na kumekuwa na ongezeko la mahitaji ya matrekta hivyo karakana hiyo ina umuhimu wa pekee katika kufanikisha lengo la Serikali la kujitegemea kwa chakula.
Kwa hivyo aliwataka watumishi wa karakana hiyo kuienzi karakana kwa kuiweka katika mazingira mazuri tofauti na sasa ambapo mazingira yake hayaridhishi.
“Sikupendezewa na namna vifaa vilivyowekwa pamoja na mazingira ya karakana yalivyo kwa ujumla”alieleza Dk. Shein na kuwakumbusha watumishi hao kuthamini dhamana waliyokabidhiwa kuiendesha karakana hiyo.
Aliongeza kuwa katika hali aliyoikuta ingawa kuna maswali mengi kuliko majibu lakini cha kushangaza mambo yote hayo majibu yake yamo ndani ya uwezo wa menejimenti.
Aliwaeleza watumishi hao pamoja na viongozi wa Wizara ya Kilimo wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wake Ndg. Juma Ali Juma kuwa ametembelea karakana hiyo ili kuona, kusikiliza maoni yao na kuangalia namna ya kuiimarisha.
Aliwataka watumishi wa karakana hiyo kubadilika kwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo na kusisitiza kuwa hawana budi kuziunga mkono hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kuimarisha karakana hiyo.
“Sisi Serikali tumedhamiria kuibadilisha karakana hii iwe ya kisasa hivyo nanyi lazima mubadilike kwa kufanya kazi kwa bidii, kujenga upendo na ushirikiano kati yenu” Dk. Shein alisisitiza.
Katika mkutano huo watumishi wengi waliopata fursa kutoa maoni yao kwa Mhe Rais walilalamikia maslahi duni, mazingira ya kazi yasiyoridhisha pamoja na kukosa fursa za mafunzo kumudu majukumu yao ya kila siku.
Watumishi hao walieleza kuwa kutokana na maendeleo ya tekinolojia vifaa vipya vya kilimo yakiwemo matrekta yanatumia tekinolojia tofauti hivyo inawawia vigumu kumudu majukumu yao ipasavyo kwa kuwa wengi wao wamesoma miaka mingi na wamekuwa hawapati fursa za kuongeza ujuzi.
Akitoa maelezo kabla ya kumkaribisha Mheshimiwa Rais, Naibu Katibu Mkuu Kilimo na Maliasili Ndg. Juma Ali Juma alieleza malalamiko ya watumishi ikiwemo ya mishahara na posho za likizo Wizara inayashughulikia hatua kwa hatua.
Kwa upande wa mafunzo alikiri kuwa lipo tatizo la watumishi wa karakana kukosa mafunzo lakini kwa nyakati tofauti mafundi kutoka nje huitwa kufanyakazi na watumishi hao hivyo kuongeza ujuzi wao.
Akiwa katika karakana hiyo alitembelea sehemu mbalimbali zikiwemo matengenezo ya matrekta, utengenezaji wa vipuri pamoja ghala.
Katika ziara hiyo Dk. Shein alifuatana na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Maalim Abdulla Mwinyi Khamis na watendaji wengine wa Serikali.
Karakana ya matrekta Mbweni ilianzishwa mwaka 1966 na imekuwa kitovu cha matengenezo ya matrekta, vifaa vingine vya kilimo pamoja na kutengeneza viputi vya baadhi ya mitambo.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822