STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 13 Agosti, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza tena umuhimu wa viongozi na watendaji wakuu katika sehemu za kazi kufanya vikao na watumishi ili kuimarisha mazingira ya kazi na kuleta ufanisi katika utendaji.
Akizungumza na watumishi wa Karakana ya Serikali ya Matrekta na watumishi wengine wa wizara ya Kilimo na Maliasili leo mara baada ya kutembelea karakana hiyo Dk. Shein alieleza kuwa malalamiko mengi yaliyotolewa na watumishi katika kikao hicho yanadhihirisha kuwa uongozi wa karakana haukutani na watumishi.
“Ni lazima watumishi wapewe fursa za kutoa maoni yao na menejimenti hazina budi kusikiliza maoni hayo na kuyafanyia kazi” alieleza Dk. Shein na kusisitiza kuwa viongozi wasijenge fikra kuwa watumishi wanaosema ukweli ni wakorofi na wakati wingine kuwachukulia hatua.
Alieleza kuwa si vyema malalamiko ya watumishi yakasubiri ujio wa kiongozi wa kitaifa na kutanabahisha kuwa hali hiyo inakaribisha majungu na fitna katika sehemu za kazi.
Dk Shein alibainisha kuwa ni kweli wapo wakuu wa maeneo ya kazi wanaopenda kila siku kusikia maneno mazuri kutoka kwa watumishi walio chini yao japokuwa ni kinyume na hali halisi lakini katika zama za sasa za demokrasia alisema jambo hilo haliwezekani tena.
Kwa hivyo alitahadharisha viongozi na watendaji wa aina hiyo dhidi ya kuwachukulia hatua watumishi pasi na kufuata Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2001 ambayo mbali ya kuainisha makosa lakini pia imeweka aina na viwango vya adhabu kwa watumishi wanaofanya makosa.
“Kuna Sheria ya Utumishi wa Umma ambayo imeweka wazi haki mbalimbali za watumishi na adhabu za makosa hivyo viongozi na watendaji waliopewa mamlaka lazima wazifuate sheria hizo” alisema Dk. Shein na kuongeza kuwa viongozi “wasitumie ubabe”.
Dk. Shein alisema mtumishi wa umma anapaswa kupewa maslahi yake kwa mujibu wa sheria ya Utumishi wa Umma bila hata yeye kulazimika kudai na kusisitiza kuwa huo ni wajibu wa watendaji kukahikisha kuwa kila mtumishi anapati haki yake bila vikwazo vyo vyote.
Katika mkutano huo watumishi wengi waliopata fursa kutoa maoni yao kwa Mhe Rais walilalamikia maslahi duni, mazingira ya kazi yasiyoridhisha pamoja na kukosa fursa za mafunzo kumudu majukumu yao ya kila siku.
Watumishi hao walieleza kuwa kutokana na maendeleo ya tekinolojia vifaa vipya vya kilimo yakiwemo matrekta yanatumia tekinolojia tofauti hivyo inawawia vigumu kumudu majukumu yao ipasavyo kwa kuwa wengi wao wamesoma miaka mingi na wamekuwa hawapati fursa za kuongeza ujuzi.
Karakana ya matrekta Mbweni ilianzishwa mwaka 1966 na imekuwa kitovu cha matengenezo ya matrekta, vifaa vingine vya kilimo pamoja na kutengeneza viputi vya baadhi ya mitambo.