Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Wabunge, wawakilishi CUF watakiwa kuchangia miradi ya chama

$
0
0
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akimkabidhi funguo za gari Mwenyekiti wa CUF, Wilaya ya Mkoani, Rashid Saleh. Gari hiyo imetolewa kwa ajili ya shughuli za chama. Kushoto ni Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.        (Picha na Ali Hamad, OMKR).
 
Na Khamis Haji OMKR
 
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad amewataka Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka chama hicho wasijisahau na watekeleze wajibu wao wa kuchangia miradi ya chama na kufanikisha malengo kiliyojiwekea kwa katika wakati muafaka.

 Amesema hayo huko Changaweni, Wilaya ya Mkoani Kusini Pemba, wakati wa uzinduzi wa ofisi mpya ya chama Wilaya ya Mkoani,  ambapo pia chama Wilaya hiyo ilikabidhiwa gari kwa ajili ya kufanikisha shughuli za chama.
Katibu Mkuu huyo alisema CUF kinatekeleza mpango wake wa kujenga ofisi za kisasa za Wilaya, Majimbo na Matawi kama hatua moja wapo ya kuzifanya kuwa za kisasa na zinazolingana na hadhi ya chama hicho.
Maalim Seif alisema CUF ni chama chenye nguvu kubwa na hivi sasa kimechukua hatua mbali mbali katika kujiandaa kukamata Serikali ya Zanzibar na ya Jamhuri ya Muuungano katika uchaguzi mkuu ujao, hivyo viongozi na wanachama ni jukumu lao kuunga mkono hatua hizo.

Amesema azma hiyo itafikiwa iwapo wanachama na viongozi wote watakuwa tayari kujituma na kuonesha ari na moyo wa kuchangia kikamilifu kazi za chama, ikiwemo ujenzi wa ofisi za kisasa.
Hata hivyo, Maalim Seeif amesema licha ya kuwepo mwamko mkubwa kwa baadhi ya viongozi na wanachama kuchangia ujenzi wa ofisi hizo, bado wapo baadhi ya viongozi wamekuwa wagumu kufanikisha mipango hiyo.
Amesema juhudi zilizochukuliwa na viongozi na wanachama wa Wilaya ya Mkoani kukamilisha ujenzi wa ofisi ya kisasa ni za kupigiwa mfano na zinapaswa kuigwa na viongozi katika maeneo mengine.
Aidha, alisema bado haridhishwi na kasi ndogo ya ujenzi wa ofisi ya chama Wilaya ya Wete, ambao umekuwa ukienda kwa mwendo wa kusua sua kutokana na baadhi ya viongozi kutotekeleza wajibu wao wa kuchangia ujenzi kikamilifu.
“Nauagiza uongozi wa Wilaya ya Wete kuhakikisha Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanachangia ujenzi kikamilifu na jengo lao liwe limekamilika ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu”, alisema.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akihutubia katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na CUF alisema busara inahitajika kuiepusha nchi kuingia katika mgogoro wa kisiasa kutokana na hali halisi iliyojitokeza katika suala la kutafuta Katiba mpya.
Katika mkutano huo uliofanyika katika skuli ya Ng’ombeni, Wilaya ya Mkoani, Mwenyekiti Lipumba alikabidhi kadi kwa wanachama wapya 1,035 waliojiunga na chama kutoka Wilaya moja ya Mkoani.
Profesa Lipumba amesema ni wazi iwapo hatua mbadala hazitachukuliwa kuepusha kasoro zilizojitokeza kabla ya uchaguzi mkuu hakuna uhakika uchaguzi huo kufanyika kwa salama na amani.
Amesema hivi sasa Bunge maalum la Katiba linaendelea bila ya wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), huku wabunge wa CCM wakibadilisha kanuni na kuingiza mambo wanayotaka kwenye rasimu ya Katiba kwa maslahi ya chama chao na sio ya wananchi walio wengi.
 Mwenyekiti huyo amesema mbali na mkwamo unaolikabili Bunge Maalum, hakuna uhakika wa kupatikana daftari la wapiga kura katika wakati muafaka kabla ya uchaguzi mkuu.
Alieleza kuwa wananchi wapatao milioni 23 wanahitaji kuandikishwa katika daftari hilo zoezi ambalo linahitaji shilingi bilioni 293, wakati fedha zilizoidhinishwa kwenye bajaeti ya serikali kwa ajili ya shughuli hiyp ni shilingi bilioni saba.
“Natoa wito kwa Rais Kikwete ayatazame mambo haya kwa uhalisia wake, asitishe Bunge Maalum, huu ni wakati wa kutumia busara kwa sababu hili ni jambo zito”’, alisema Profesa Lipumba.
Mkutano huo pia umehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Magdalena Sakaya ambaye amewahimza wanachama wa CUF kisiwani Pemba kuzidi kuwa imara ili wakiwezeshe chama hicho kushika dola katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>