Na Kauthar Abdalla
JUMUIYA ya maradhi yasiyoambukiza Zanzibar, inakusudia kufanya uchunguzi wa awali wa kansa ya shingo ya kizazi kwa wanawake walio na umri wa miaka 35 na kuendelea.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mpendae, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Ali Mansour Vuai, alisema wanawake wengi wanaathiriwa na ugonjwa huo kutokana na dalili zake kutojitokeza mapema.
Alisema kuna jumuiya mbali mbali zinazoshughulikia maradhi yasiyoambukiza kama presha na kisukari lakini hakuna jumuiya ambayo inashughulika na saratani ya shingo ya kizazi kwa sababu ni maradhi ambayo yana usiri mkubwa kwa wanawake.
Alisema ugonjwa huo una hatari kubwa ya kuwapotezea maisha wanawake kwani unahitaji uchunguzi wa kina na una gharimu fedha nyingi kutibiwa.
Pia alisema jumuiya hiyo inafanya kazi ya kitaifa lakini inahitaji msaada wa kijamii ili ili ifanikiwe malengo yake.
Aliiomba jamii kuunga mkono utafiti huo pamoja na kuisaidia jumuiya kufikia malengo yake.