Na Tatu Makame
MKUU wa kitengo cha mazao ya biashara kutoka Idara ya Misitu na Maliasili Zisizorejesheka, Is-haka Mohamed Abdulwakil, ametoa wito kwa wakulima wa karafuu kuwa na utamaduni wa kuitunza mikarafuu baada ya mavuno.
Wito huo aliutoa ofisini kwake Maruhubi,wakati akizungumza na mwanduishi wa habari hizi.
Alisema kumejitokeza mtindo wa baadhi ya wakulima kutokuwa na utamaduni wa kuitunza mikarafuu baada ya mavuno na kusababisha mavuno ya karafuu kupungua msimu hadi msimu.
Alisema serekali inatumia gharama kubwa kuendeleza zao la karafuu, hivyo ni wajibu wa wakulima kuhakikisha wakati wote mikarafuu inakuwa safi.
Aidha aliwahimiza wakulima wapya wa mikarafuu kuomba kupatiwa miche ya mikarafuu ambayo hutolewa bure ili kuhakikisha kilimo cha mikarafuu kinarejea katika asili yake.
Alisema kutokana umuhimu wa zao hilo wameandaa mafunzo maalum yatakayowasaidia wakulima kujua namna ya kuitunza
na kuihifadhi mikarafuu.
Nae Ofisa wa uzalishaji miche kutoka idara hiyo, Rashid Nasor Rashid, alisema mikakati yao ni kuhakikisha kila mwaka wanazalisha miechi milioni moja na kuigawa kwa wakulima.