Na Fatina Mathias, Dodoma
Rais Jakaya Kikwete, ameshangazwa na ufaulu wa chini katika wilaya za Chemba na Kondoa mkoani Dodoma na kuwataka viongozi kukaa chini na kujiuliza sababu ya kushuka kwa ufaulu huo.
Agizo hilo alilitoa kwa nyakati tofauti akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoa wa Dodoma.
Alisema kiwango cha ufaulu nchini kimekuwa kikiongezeka lakini wilaya hizo zimeendelea kuwa chini kielimu.
"Mwaka jana katika wilaya ya Kondoa ufaulu katika darasa la saba ulikuwa asilimia 23 na kwa kidato cha nne ulikuwa asilimia 46 ambapo katika wilaya ya Chemba kiwango cha ufaulu ni asilimia 19 wakati lengo lililopo ni kuinua ufaulu hadi kufikia asilimia 60 ili mwakani wafike kwenye asilimia 80,"alisema.
Kuhusu migogoro ya mipaka,aliahidi kukutana na Waziri Mkuu na viongozi wengine wenye dhamana ili waweze kulipatia ufumbuzi wa kudumu kwa kuwa katika ziara yake alipokea vilio vya migogoro hiyo.
Alisema wakati akipita katika kijiji cha Haneti, wananchi walisimamisha msafara wake na kueleza kilio chao cha mgogoro wa mipaka.
Aidha aliiagiza halmashauri ya wilaya ya Chemba m kuhakikisha inatenga ardhi kwa ajili ya Shirika la Nyumba (NHC) ili liweze kujenga nyumba bora kwa ajili ya watumishi.
Alisema wakiwapa ardhi NHC watawajengea nyumba bora na hivyo itaondoa visingizio vya watumishi kwenda kukaa wilaya
nyingine ya Kondoa.
Alisema katika maeneo ambayo NHC wamejenga makazi wamefanya vizuri kwa kuwa yatasaidia pia kuifanya wilaya
kuonekana na kupangika vizuri.
Aidha alisema hali hiyo itawafanya wafanyakazi wasipate adha ya kupanga nyumba ambazo mazingira yake hayaridhishi.
Aidha alisema eneo la ujenzi wa hospitali limepatikana na NHC wamekabidhiwa ili waweze kujenga na atawasaidia kulisemea
suala hilo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia, alisifu afanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa ilani ya
uchaguzi ya CCM na kumpongeza Rais na serikali yake kwa kufanikisha hilo.